Agano la Kale

Agano Jipya

Nehemia 12:30-47 Biblia Habari Njema (BHN)

30. Makuhani na Walawi walijitakasa, pia waliwatakasa watu, malango na ukuta.

31. Niliwakusanya viongozi wote wa Yuda kwenye ukuta na kutenga waimbaji katika makundi mawili makubwa yaliyoimba nyimbo za shukrani wakiwa katika maandamano. Kundi moja lilielekea upande wa kulia wa ukuta hadi kwenye Lango la Takataka.

32. Waimbaji hao walifuatiwa na Hoshaya akiwa pamoja na nusu ya viongozi wa Yuda.

33. Pamoja naye walikwenda Azaria, Ezra, Meshulamu,

34. Yuda, Benyamini, Shemaya na Yeremia.

35. Wazawa wafuatao wa makuhani walikuwa na tarumbeta: Zekaria, mwana wa Yonathani, mwana wa Shemaya aliyekuwa mwana wa Matania, mwana wa Mikaya, mwana wa Zakuri, mwana wa Asafu.

36. Ndugu zake wafuatao waliimba kwa ala za muziki za mfalme Daudi, mtu wa Mungu, yaani Shemaya, Azareli, Milalai, Gilalai, Maai, Nethaneli, Yuda na Hanani, walitanguliwa na Ezra mwandishi.

37. Kwenye Lango la Chemchemi walipanda ngazi kuelekea mji wa Daudi, wakaipita Ikulu ya Daudi, na kuelekea nyuma kwenye ukuta hadi kwenye Lango la Maji, mashariki ya mji.

38. Kundi lingine lililoimba nyimbo za shukrani lilielekea upande wa kushoto juu ya ukuta. Mimi nilifuatana na kundi hili pamoja na nusu ya watu. Tulipitia Mnara wa Tanuri hadi kwenye Ukuta Mpana.

39. Na kutoka hapo, tulipitia Lango la Efraimu, Lango la Yeshana, Lango la Samaki, Mnara wa Hananeli, Mnara wa Mia Moja mpaka kwenye Lango la Kondoo. Tulimalizia maandamano yetu kwenye Lango la Gereza.

40. Hivyo, makundi yote mawili yaliyokuwa yanaimba nyimbo za shukrani yalisimama katika nyumba ya Mungu, pamoja nami na nusu ya viongozi;

41. hata na makuhani waliokuwa na tarumbeta: Eliakimu, Maaseya, Miniamini, Mikaya, Eliehoenai, Zekaria na Hanania.

42. Hao walifuatwa na Maaseya, Shemaya, Eleazari, Uzi, Yehohanani, Malkiya, Elamu na Ezeri. Waimbaji waliimba wakiongozwa na Yezrahia.

43. Siku hiyo, watu walitoa tambiko nyingi na kufurahi kwani Mungu aliwafanya wawe na furaha kubwa. Pia wanawake na watoto, wote walifurahi. Vigelegele vya furaha toka mjini Yerusalemu vilisikika mbali.

44. Wakati huo walichaguliwa watu wa kutunza vyumba vya ghala ambamo matoleo kwa ajili ya hekalu yalitunzwa, malimbuko ya kwanza, zaka na kuyakusanya kutoka mashamba ya miji, kwa ajili ya makuhani na Walawi kama ilivyotakiwa na sheria. Watu wote waliwafurahia makuhani na Walawi waliohudumu,

45. kwa sababu walifanya ibada ya Mungu wao na ibada ya utakaso, kama waimbaji walivyoimba hata walinzi wa malango kulingana na agizo la mfalme Daudi na Mfalme Solomoni mwanawe.

46. Tangu wakati wa mfalme Daudi na Asafu kulikuweko kiongozi wa waimbaji, na kulikuwako nyimbo za sifa na shukrani kwa Mungu.

47. Watu wote wa Israeli, tangu wakati wa Zerubabeli na Nehemia, walitoa matoleo ya kila siku ambayo yaliwatunza waimbaji walinda malango. Zaidi ya yote, watu wa Israeli walitoa matoleo kwa ajili ya Walawi, nao Walawi wakatenga sehemu kwa ajili ya wazawa wa Aroni.

Kusoma sura kamili Nehemia 12