Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 47:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Basi, Yosefu akaenda kwa Farao, akamwambia, “Baba yangu na ndugu zangu pamoja na kondoo, ng'ombe na mali yao yote, wamefika kutoka nchi ya Kanaani. Sasa wako katika eneo la Gosheni.”

2. Yosefu alikuwa amewachukua ndugu zake watano, akawajulisha kwa Farao.

3. Farao akawauliza, “Kazi yenu ni nini?” Wakamjibu, “Bwana, sisi watumishi wako ni wachungaji, kama walivyokuwa babu zetu.”

4. Kisha wakamwambia Farao, “Sisi watumishi wako tumekuja kukaa kama wageni humu nchini kwa kuwa njaa ni kali huko Kanaani na hakuna tena malisho kwa mifugo yetu. Hivyo, bwana, tunakuomba, sisi watumishi wako, uturuhusu kukaa katika eneo la Gosheni.”

5. Farao akamwambia Yosefu, “Baba yako na ndugu zako wamekujia wewe.

6. Nchi yote ya Misri iko chini yako; wape baba yako na ndugu zako sehemu bora ya nchi hii. Waache wakae katika eneo la Gosheni. Na iwapo unawafahamu watu stadi miongoni mwao, wateue wawe waangalizi wa mifugo yangu.”

7. Kisha, Yosefu akamleta baba yake Yakobo kumwamkia Farao; naye Yakobo akampa Farao baraka zake.

8. Farao akamwuliza Yakobo, “Umri wako ni miaka mingapi?”

9. Yakobo akamjibu, “Umri niliojaliwa kama msafiri ni miaka 130. Miaka hiyo imekuwa michache na iliyojaa mateso, tena haijafikia idadi ya miaka waliyoishi wazee wangu kama wasafiri.”

10. Kisha Yakobo akambariki Farao, akaondoka.

11. Basi, Yosefu akawapa baba yake na ndugu zake eneo la Ramesesi lililo bora kabisa katika nchi ya Misri, liwe makao yao, nao wakalimiliki kama alivyoagiza Farao.

Kusoma sura kamili Mwanzo 47