Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 45:4-11 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Yosefu akawaambia ndugu zake, “Tafadhali, sogeeni karibu nami.” Walipomkaribia, akawaambia, “Mimi ndiye ndugu yenu Yosefu, mliyemwuza Misri.

5. Lakini sasa msifadhaike wala kujilaumu kwa kuniuza. Mungu ndiye aliyenileta huku niwatangulie, ili niyaokoe maisha ya watu.

6. Huu ni mwaka wa pili tu wa njaa nchini, na bado kuna miaka mitano zaidi ambapo watu hawataweza kulima wala kuvuna mavuno.

7. Mungu alinileta huku niwatangulie, ili kusalimisha maisha yenu mbaki hai nchini na kuwakomboa kwa ukombozi mkubwa.

8. Kwa hiyo, si nyinyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Ndiye aliyenifanya kama baba kwa Farao, msimamizi wa nyumba yake yote na mtawala wa nchi yote ya Misri.

9. Basi, fanyeni haraka, mwende kwa baba na kumwambia, ‘Yosefu, mwana wako, anasema: Mungu amenifanya kuwa mkuu wa nchi yote ya Misri. Basi, usikawie kuja kwangu.

10. Utakaa karibu nami katika eneo la Gosheni: Wewe, wana wako na wajukuu wako, mifugo yako na mali yako yote.

11. Utakapokuwa Gosheni, mimi nitakutunza wewe, jamaa yako pamoja na mifugo yako ili msije mkafa njaa, kwani bado miaka mitano zaidi ya njaa.’”

Kusoma sura kamili Mwanzo 45