Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 44:13-28 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Hapo wakayararua mavazi yao kwa huzuni. Kila mmoja wao akambebesha punda wake mzigo wake, wakarudi mjini.

14. Yuda na nduguze wakafika nyumbani kwa Yosefu naye Yosefu alikuwapo bado nyumbani. Basi, wakamwinamia kwa heshima,

15. naye Yosefu akawauliza, “Kwa nini mmefanya hivyo? Je hamjui kwamba mtu kama mimi ninao uwezo wa kubashiri?”

16. Yuda akamjibu, “Tukuambie nini bwana? Tuseme nini kuonesha kwamba hatuna hatia? Mungu ameyafichua makosa yetu, sisi watumishi wako. Sasa sote tu watumwa wako, sisi pamoja na yule aliyepatikana na kikombe chako.”

17. Lakini Yosefu akasema, “La! Mimi siwezi kufanya hivyo! Yule tu aliyepatikana na kikombe changu ndiye atakayekuwa mtumwa wangu. Nyinyi wengine wote rudini kwa amani kwa baba yenu.”

18. Ndipo Yuda akamkaribia Yosefu na kumwambia, “Bwana, nakuomba uniruhusu mimi mtumishi wako, nijitetee mbele yako kwa maneno machache; ninakusihi usinikasirikie, kwani wewe ni kama Farao mwenyewe.

19. Bwana, wewe ulituuliza kama tuna baba au ndugu,

20. nasi tukakueleza kwamba tunaye baba, naye ni mzee, na kwamba tunaye ndugu mwingine mdogo aliyezaliwa wakati wa uzee wa baba yetu. Kaka yake huyo kijana amekwisha fariki, na huyo mdogo ndiye peke yake aliyebaki wa mama yake; na mzee wetu anampenda sana kijana huyo.

21. Bwana, ulituagiza sisi watumishi wako kumleta huyo mdogo wetu upate kumwona.

22. Tukakueleza kwamba huyo kijana hawezi kuachana na baba yake, kwa sababu akifanya hivyo baba yake atakufa.

23. Lakini wewe bwana ukatuambia kwamba kama hatutakuja na ndugu yetu mdogo, hutatupokea tena.

24. “Tuliporudi nyumbani kwa mtumishi wako, baba yetu, tulimwarifu ulivyotuagiza, bwana.

25. Naye alipotuambia tuje tena huku kununua chakula,

26. tulimwambia, ‘Hatuwezi kwenda, isipokuwa tu kama ndugu yetu mdogo atakwenda pamoja nasi; kama hatakwenda pamoja nasi hatuwezi kupokelewa na yule mtu.’

27. Basi, baba yetu, mtumishi wako, akatuambia, ‘Mnajua kwamba mke wangu Raheli alinizalia wana wawili:

28. Mmoja alitoweka, nami nikasema, bila shaka ameraruliwa vipandevipande na mnyama wa porini, maana sijapata kumwona tena.

Kusoma sura kamili Mwanzo 44