Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 42:7-18 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Yosefu alipowaona kaka zake akawatambua, lakini akajifanya kana kwamba hawafahamu, akasema nao kwa ukali. Akawauliza, “Mmetoka wapi nyinyi?” Wakamjibu, “Tumetoka nchini Kanaani, tumekuja kununua chakula.”

8. Ingawa Yosefu aliwatambua kaka zake, wao hawakumtambua.

9. Akakumbuka ndoto zake za zamani juu ya kaka zake, akawaambia, “Nyinyi ni wapelelezi. Mmekuja kupeleleza udhaifu wa nchi yetu.”

10. Wao wakamjibu, “Sivyo, bwana wetu. Sisi watumishi wako tumekuja kununua chakula.

11. Sisi ni ndugu, wana wa baba mmoja. Sisi ni watu waaminifu, na wala si wapelelezi.”

12. Lakini Yosefu akasisitiza, “Sivyo! Mmekuja hapa ili kupeleleza udhaifu wa nchi yetu.”

13. Wakamwambia, “Sisi, watumishi wako, tuko ndugu kumi na wawili, wana wa mtu mmoja, mwenyeji wa nchi ya Kanaani. Mdogo wetu amebaki na baba nyumbani, na ndugu yetu mwingine ni marehemu.”

14. Lakini Yosefu akawaambia, “Ni kama nilivyosema: Nyinyi ni wapelelezi tu.

15. Hivi ndivyo mtakavyojaribiwa: Naapa kwa jina la Farao, kwamba hamtatoka hapa mpaka mdogo wenu atakapokuja.

16. Mtumeni mmoja wenu akamlete huyo ndugu yenu mdogo, wakati wengine wenu wanamngoja gerezani. Hapo ndipo maneno yenu yatakapojulikana ukweli wake. La sivyo, naapa kwa jina la Farao kwamba nyinyi ni wapelelezi.”

17. Kisha akawatia wote gerezani kwa muda wa siku tatu.

18. Siku ya tatu Yosefu akawaambia, “Kwa kuwa mimi ni mcha Mungu, fanyeni hivi ili mpate kuishi:

Kusoma sura kamili Mwanzo 42