Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 42:28-38 Biblia Habari Njema (BHN)

28. Akawaambia ndugu zake, “Fedha yangu imerudishwa. Hii hapa mdomoni mwa gunia langu!” Waliposikia hayo, wakafa moyo. Wakatazamana huku wanatetemeka na kuulizana, “Ni jambo gani hili alilotutendea Mungu?”

29. Walipowasili nchini Kanaani kwa baba yao Yakobo, walimsimulia yote yaliyowapata, wakamwambia,

30. “Mkuu wa nchi ile alisema nasi kwa ukali, na kutushuku kwamba sisi ni wapelelezi nchini mwake.

31. Lakini sisi tulimweleza kuwa sisi ni watu waaminifu, na wala si wapelelezi.

32. Tulimweleza kuwa sisi tuko ndugu kumi na wawili wa baba mmoja, na kwamba mmoja wetu ni marehemu na yule mdogo yuko nyumbani nchini Kanaani pamoja na baba yetu.

33. Ndipo mkuu wa nchi hiyo akatuambia, ‘Hivi ndivyo nitakavyotambua kama kweli nyinyi ni watu waaminifu: Mwacheni kwangu ndugu yenu mmoja, nanyi wengine mpeleke nafaka nyumbani kwa jamaa zenu wenye njaa.

34. Kisha mleteni kwangu huyo ndugu yenu mdogo, na hapo nitajua kuwa nyinyi si wapelelezi, ila ni watu waaminifu. Mkifanya hivyo nitamwacha huru ndugu yenu, nanyi mtaruhusiwa kufanya biashara katika nchi hii.’”

35. Walipokuwa wanamimina nafaka kutoka magunia yao, walishangaa kuona kila mmoja wao amerudishiwa kifuko chake na fedha ndani ya gunia lake. Walipoona hayo, wote pamoja na baba yao, wakashikwa na hofu.

36. Baba yao Yakobo, akawaambia, “Mnanipokonya watoto wangu! Yosefu hayuko; Simeoni hayuko; sasa mnataka kumchukua na Benyamini. Yote hayo yamenipata!”

37. Hapo Reubeni akamwambia baba yake, “Nisipomrudisha Benyamini, waue wanangu wawili. Mwache Benyamini mikononi mwangu, nami nitamlinda na kumrudisha kwako.”

38. Lakini baba yake akamjibu, “Mwanangu hatakwenda nanyi; ndugu yake amekwisha fariki, naye peke yake ndiye aliyebaki. Mimi ni mzee mwenye mvi ikiwa kijana huyu atapatwa na madhara yoyote katika safari mtakayofanya basi, mtaniua kwa huzuni.”

Kusoma sura kamili Mwanzo 42