Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 41:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Baada ya miaka miwili mizima, Farao aliota ndoto: Alijikuta amesimama kando ya mto Nili,

2. akaona ng'ombe saba wazuri na wanono wakitoka mtoni na kula nyasi.

3. Halafu, baada ya hao, ng'ombe wengine saba waliokonda sana wakatoka katika mto Nili, wakaja na kusimama karibu na wale ng'ombe wazuri na wanono, kando ya mto.

4. Hao ng'ombe waliokonda sana wakawala wale wengine saba wazuri na wanono. Hapo Farao akaamka usingizini.

5. Alipolala tena, akaota mara ya pili. Aliona masuke saba makubwa na mazuri yanachipuka katika bua moja.

6. Halafu, baada ya hayo, masuke mengine saba membamba na yaliyokaushwa na upepo mkavu wa jangwani yakatokeza.

7. Hayo masuke saba membamba yakayameza yale masuke saba makubwa yaliyojaa nafaka. Basi, Farao alipoamka akagundua kuwa ilikuwa ndoto.

8. Kulipokuwa asubuhi, Farao akiwa na wasiwasi sana, aliwaita wachawi wote wa Misri, na wenye hekima, akawaambia ndoto zake, lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kumtafsiria ndoto hizo.

9. Ndipo, yule mtunza vinywaji mkuu akamwambia Farao, “Leo nayakumbuka makosa yangu!

10. Wakati ule ulipotukasirikia sisi watumishi wako, mimi na mwoka mikate mkuu, ulitufungia ndani ya ngome ya mkuu wa kikosi cha ulinzi.

11. Usiku mmoja tuliota ndoto, kila mmoja ndoto yake tofauti.

12. Basi, kijana mmoja Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa kikosi cha ulinzi, alikuwa pamoja nasi kifungoni. Tulipomsimulia ndoto zetu, yeye aliweza kututafsiria kila mmoja wetu kulingana na ndoto yake.

13. Alivyotafsiri ndivyo ilivyotokea: Mimi nikarudishwa kazini kwangu, na yule mwoka mikate mkuu akatundikwa mtini.”

Kusoma sura kamili Mwanzo 41