Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 33:10-20 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Yakobo akamwambia, “La! Kama kweli umekubali kunipokea, basi, nakusihi uipokee zawadi yangu. Hakika, kuuona uso wako ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa vile ulivyonipokea kwa wema mkubwa.

11. Basi, nakuomba uikubali zawadi niliyokuletea, kwa sababu hata mimi pia Mungu amenineemesha, nami ninayo mali nyingi.” Ndivyo Yakobo alivyomshawishi Esau, naye akaipokea zawadi yake.

12. Esau akasema, “Haya! Tuendelee na safari yetu; mimi nitakutangulia.”

13. Lakini Yakobo akamwambia, “Bwana wangu, wewe unajua kwamba watoto hawa ni wachanga, na kwamba mifugo hii inanyonyesha, nami sina budi kuitunza; kama wanyama hawa watapelekwa mbio kwa siku moja, wote watakufa.

14. Basi, nakuomba utangulie, nami nitafuata polepole kadiri ya mwendo wa wanyama na watoto, mpaka nitakapokufikia huko Seiri.”

15. Hapo Esau akasema, “Heri nikuachie baadhi ya watu wangu.” Lakini Yakobo akasema, “Kuna haja gani ya kufanya hivyo? Yanitosha kwamba mimi nimepata fadhili yako, ewe bwana wangu.”

16. Basi, siku hiyo Esau akaanza safari ya kurudi Seiri.

17. Lakini Yakobo akasafiri kwenda Sukothi, na huko akajijengea nyumba na vibanda kwa ajili ya wanyama wake. Kwa sababu hiyo, mahali hapo pakaitwa Sukothi.

18. Kutoka Padan-aramu, Yakobo alifika salama mjini Shekemu, katika nchi ya Kanaani, akapiga kambi yake karibu na mji huo.

19. Sehemu hiyo ya ardhi ambako alipiga kambi aliinunua kutoka kwa wazawa wa Hamori, baba yake Shekemu, kwa vipande 100 vya fedha.

20. Huko, akajenga madhabahu na kupaita Mungu ni Mungu wa Israeli.

Kusoma sura kamili Mwanzo 33