Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 31:21-38 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Basi, Yakobo akachukua mali yake yote, akatoroka. Baada ya kuvuka mto Eufrate, alielekea Gileadi, nchi ya milima.

22. Siku tatu baadaye, Labani alijulishwa kwamba Yakobo amemtoroka.

23. Basi, Labani akawachukua ndugu zake, akamfuata Yakobo kwa muda wa siku saba, akamkuta milimani, nchini Gileadi.

24. Lakini usiku, Mungu akamtokea Labani, Mwaramu, katika ndoto, akamwambia, “Jihadhari! Usimwambie Yakobo neno lolote lile, jema au baya.”

25. Basi, Labani akamfikia Yakobo. Wakati huo Yakobo alikuwa amepiga kambi yake milimani. Labani naye, pamoja na ndugu zake, akapiga kambi yake kwenye milima ya Gileadi.

26. Ndipo Labani akamwambia Yakobo, “Umefanya nini? Mbona umenidanganya, ukawachukua binti zangu kama mateka vitani?

27. Kwa nini ulitoroka kisiri, ukanihadaa, wala hukuniarifu ili nipate kukuaga kwa shangwe, nyimbo, matari na vinubi?

28. Mbona hukunipa fursa ya kuwabusu kwaheri binti zangu na wajukuu zangu? Kweli umetenda kipumbavu!

29. Nina uwezo wa kukudhuru; lakini Mungu wa baba yako alinitokea usiku wa kuamkia leo, akanitahadharisha akisema, ‘Jihadhari! Usimwambie Yakobo neno lolote lile, jema au baya’.

30. Najua ulitoroka kwa sababu ya hamu kubwa ya kurudi nyumbani kwa baba yako. Lakini kwa nini uliiba vinyago vya miungu yangu?”

31. Yakobo akamjibu, “Niliogopa kwa sababu nilidhani ungelininyanganya binti zako.

32. Lakini utakayempata na vinyago vya miungu yako asiishi! Mbele ya hawa ndugu zetu, onesha chochote kilicho chako, ukichukue.” Yakobo hakujua kwamba Raheli alikuwa ameiba vinyago vya miungu ya Labani.

33. Basi, Labani akatafuta vinyago hivyo vya miungu yake katika hema la Yakobo, la Lea na la wale wajakazi wawili; lakini hakuvipata. Akatoka katika hema la Lea na kuingia hema la Raheli.

34. Raheli alikuwa amevichukua hivyo vinyago, akavificha chini ya matandiko ya ngamia na kuketi juu yake. Labani akavitafuta katika hema lote; lakini hakuvipata.

35. Ndipo Raheli akamwambia baba yake, “Samahani baba, usiudhike, kwani siwezi kusimama mbele yako kwa sababu nimo katika siku zangu.” Basi, Labani akavitafuta vinyago vya miungu yake, lakini hakuvipata.

36. Ndipo Yakobo akakasirika, akamshutumu Labani akisema, “Kosa langu ni nini?

37. Je, umepata nini kilicho chako hata baada ya kuipekua mizigo yangu yote? Kiweke mbele ya ndugu zangu na ndugu zako, ili wao waamue kati yetu sisi wawili!

38. Nimekaa nawe kwa muda wa miaka ishirini; na muda huo wote kondoo wako, wala mbuzi wako hawajapata kuharibu mimba, wala sijawahi kula kondoo dume wa kundi lako.

Kusoma sura kamili Mwanzo 31