Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 30:32-43 Biblia Habari Njema (BHN)

32. Niruhusu nipite kati ya wanyama wako wote leo, nitenge katika kundi kila kondoo mwenye madoadoa na mabakamabaka, kila kondoo mweusi, na mbuzi walio na madoadoa na mabakamabaka. Huo ndio utakaokuwa ujira wangu.

33. Hivyo, siku zijazo, uaminifu wangu utaonekana waziwazi utakapokuja kuuangalia ujira wangu. Mbuzi yeyote asiye na madoadoa au mabakamabaka, au kondoo yeyote asiye mweusi akionekana katika kundi langu, huyo atakuwa ameibiwa.”

34. Labani akasema, “Vema! Na iwe kama ulivyosema.”

35. Lakini siku hiyohiyo Labani akaenda akawatenga mabeberu wote wenye milia na madoadoa, mbuzi wote majike waliokuwa na madoadoa na mabakamabaka, kila mnyama aliyekuwa na weupe mwilini mwake, na kila kondoo mweusi, akawaweka chini ya ulinzi wa wanawe.

36. Labani akajitenga na Yakobo umbali wa mwendo wa siku tatu; naye Yakobo akabaki akichunga wanyama wa Labani waliosalia.

37. Basi, Yakobo akatwaa fito mbichi za miti ya mlubna, mlozi na mwaramoni, akazibambua ili mistari myeupe ionekane katika fito hizo.

38. Akazisimamisha fito hizo alizozibambua mbele ya wanyama katika mabirika ya kunyweshea maji, mahali ambapo wanyama walikuja kunywa maji. Na kwa kuwa wanyama walichukua mimba walipokuja kunywa maji,

39. wakapata mimba mbele ya hizo fito; wakazaa wanyama wenye milia, mabakamabaka na madoadoa.

40. Yakobo akawatenga hao wanakondoo, kisha akawaelekeza kwenye wanyama wenye milia na weusi katika kundi la Labani. Kwa njia hii, Yakobo akajipatia kundi lake mwenyewe, wala hakulichanganya na lile la Labani.

41. Ikawa kila yalipofika majira ya wanyama wenye afya kuchukua mimba, Yakobo aliziweka zile fito mbele yao katika mabirika ya kunyweshea maji, ili wachukue mimba penye fito hizo.

42. Lakini hakuziweka fito hizo mbele ya wanyama dhaifu walipochukua mimba. Punde si punde, wanyama dhaifu wakawa wa Labani, na wenye afya wakawa wa Yakobo.

43. Basi, Yakobo akatajirika sana, akawa na makundi makubwa ya wanyama, watumishi wa kike na wa kiume, ngamia na punda.

Kusoma sura kamili Mwanzo 30