Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 28:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Hivyo Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akisema, “Usioe mwanamke yeyote Mkanaani.

2. Nenda Padan-aramu, nyumbani kwa babu yako Bethueli, ukaoe mmojawapo wa binti za mjomba wako Labani.

3. Mungu mwenye nguvu na akubariki upate wazawa wengi na kuongezeka, ili uwe jamii kubwa ya watu.

4. Akubariki wewe pamoja na wazawa wako kama alivyombariki Abrahamu, upate kuimiliki nchi ambamo unakaa kama mgeni; nchi ambayo Mungu alimpa Abrahamu!”

5. Basi, Isaka akamtuma Yakobo, naye akaenda Padan-aramu kwa Labani, mwana wa Bethueli, Mwaramu, kaka yake Rebeka, mama yao Yakobo na Esau.

6. Esau alitambua kwamba Isaka alikuwa amembariki Yakobo na kumtuma aende kuoa huko Padan-aramu, na ya kuwa alipombariki, alimkataza asioe mwanamke Mkanaani.

7. Alitambua pia kuwa Yakobo alimtii mama yake na baba yake, akaenda Padan-aramu.

8. Basi, Esau akafahamu kwamba baba yake hapendezwi na wanawake wa Kanaani.

9. Hivyo, mbali na wale wake zake wengine, Esau akaenda kwa Ishmaeli, mwana wa Abrahamu, akamwoa Mahalathi binti Ishmaeli, dada yake Nebayothi.

10. Yakobo aliondoka Beer-sheba, akaelekea Harani.

11. Alipofika mahali fulani, akalala hapo kwa sababu jua lilikuwa limetua. Alichukua jiwe moja la mahali hapo, akaliweka chini ya kichwa chake, akalala.

12. Aliota ndoto, na katika ndoto hiyo, aliona ngazi iliyosimamishwa duniani na ncha yake inafika mbinguni. Malaika wa Mungu walikuwa wakipanda na kushuka katika ngazi hiyo.

Kusoma sura kamili Mwanzo 28