Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 22:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Baada ya muda fulani, Mungu alimjaribu Abrahamu. Mungu alimwita, “Abrahamu!” Naye akaitika, “Naam nasikiliza.”

2. Mungu akamwambia, “Mchukue mwanao, Isaka, mwanao wa pekee umpendaye, uende mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa juu ya mlima mmojawapo nitakaokuonesha.”

3. Basi, kesho yake, Abrahamu akaamka asubuhi na mapema, akatandika punda wake, akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaka mwanawe. Akatayarisha kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, kisha akaanza safari kuelekea mahali alipoambiwa na Mungu.

4. Mnamo siku ya tatu, Abrahamu aliinua macho akapaona mahali hapo kwa mbali.

5. Akawaambia wale watumishi wake, “Ngojeni hapa na huyu punda. Mimi na mwanangu tutakwenda mpaka kule, tukamwabudu Mungu, kisha tutawarudiani.”

6. Basi, Abrahamu akazitwaa zile kuni, akamtwika Isaka mwanawe; yeye mwenyewe akachukua moto na kisu mkononi; wakaondoka pamoja.

7. Isaka akamwuliza baba yake, “Baba, moto na kuni tunazo; lakini mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa yuko wapi?”

8. Abrahamu akamjibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atatujalia mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa.” Basi, wakaendelea na safari yao.

9. Walipofika mahali ambapo Mungu alimwagiza, Abrahamu akajenga madhabahu na kupanga kuni juu yake. Kisha akamfunga Isaka mwanawe na kumlaza juu ya kuni juu ya madhabahu.

Kusoma sura kamili Mwanzo 22