Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 20:2-13 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Akiwa huko, Abrahamu alisema kuwa mkewe Sara ni dada yake. Kwa hiyo, mfalme Abimeleki wa Gerari akamchukua Sara.

3. Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto usiku, akamwambia, “Wewe utakufa kwa sababu ya mwanamke uliyemchukua, kwani ana mumewe.”

4. Abimeleki ambaye bado hakuwa amelala na Sara, akajibu, “Bwana, utawaua watu wasio na hatia.

5. Abrahamu mwenyewe ndiye aliyesema kuwa huyu ni dada yake. Tena hata Sara mwenyewe alisema kuwa Abrahamu ni kaka yake! Mimi nimefanya nilivyofanya kwa moyo mnyofu na sina hatia.”

6. Basi, Mungu akamwambia katika hiyo ndoto, “Sawa. Najua kwamba umefanya hivyo kwa moyo mnyofu, na mimi ndiye niliyekuzuia kutenda dhambi dhidi yangu; ndiyo maana sikukuruhusu umguse huyo mwanamke.

7. Sasa mrudishe huyo mwanamke kwa mume wake. Abrahamu ni nabii, naye atakuombea nawe utaishi. Lakini usipomrudisha, ujue kwa hakika kwamba wewe utakufa pamoja na watu wako wote.”

8. Basi, Abimeleki akaamka asubuhi na mapema, akawaita watumishi wake wote na kuwaeleza mambo aliyoyaona katika ndoto; nao wakaogopa sana.

9. Ndipo Abimeleki akamwita Abrahamu, akamwuliza, “Umetutendea nini? Nimekukosea nini hata ukaniletea balaa hili mimi na ufalme wangu? Umenitendea mambo yasiyostahili kutendwa.”

10. Tena Abimeleki akazidi kumwuliza, “Ni kitu gani kimekusukuma kufanya hivyo?”

11. Abrahamu akamjibu, “Nilifanya hivyo kwa kuwa hakuna amchaye Mungu mahali hapa, na kwamba mngeniua ili mumchukue mke wangu.

12. Zaidi ya hayo, kwa kweli, yeye ni dada yangu: Baba yake na baba yangu ni mmoja, lakini mama tofauti; ndiyo maana akawa mke wangu.

13. Wakati Mungu aliponifanya niiache nyumba ya baba yangu na kwenda ugenini, nilimwambia mke wangu, ‘Popote tutakapokwenda tafadhali useme kwamba mimi ni kaka yako!’”

Kusoma sura kamili Mwanzo 20