Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 19:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Wale malaika wawili wakawasili mjini Sodoma jioni. Loti ambaye alikuwa ameketi penye lango la mji wa Sodoma, alipowaona, aliinuka kuwalaki, akainama kwa heshima,

2. akasema, “Bwana zangu, karibuni nyumbani kwangu mimi mtumishi wenu. Mnaweza kunawa miguu na kulala kwangu usiku wa leo. Asubuhi na mapema mtaweza kuendelea na safari yenu.” Lakini, wao wakasema, “La! Sisi tutalala huku mtaani.”

3. Loti akawasihi sana, mwishowe wakakubali, wakageuka na kuingia nyumbani kwake. Loti akawaandalia karamu, akaoka mikate isiyotiwa chachu, wakala.

4. Lakini kabla ya kulala usiku, wanaume wote wa mji wa Sodoma, vijana kwa wazee, bila kubaki hata mmoja, wakaizingira nyumba ya Loti.

5. Wakamwita Loti na kumwuliza, “Wako wapi wale wanaume waliokuja kwako? Watoe nje. Tunataka kulala nao.”

6. Loti akatoka nje, akafunga mlango nyuma yake,

7. akawaambia, “Ndugu zangu, nawasihi msitende uovu huo.

8. Tazama, ninao binti wawili ambao bado hawajalala na mwanamume. Mniruhusu niwapeni hao wasichana muwatendee kama mpendavyo. Lakini msiwatende lolote wanaume hawa kwa sababu ni wageni wangu.”

9. Lakini wao wakasema, “Tupishe! Wewe ulikuja huku ukiwa mgeni na sasa wajifanya hakimu! Basi, tutakutenda mabaya zaidi ya hao wageni wako.” Hapo wakamsukuma Loti nyuma hata karibu wauvunje mlango wake.

10. Lakini wale wageni wakanyosha mikono yao, wakamvuta Loti ndani ya nyumba na kuufunga mlango.

Kusoma sura kamili Mwanzo 19