Agano la Kale

Agano Jipya

Mhubiri 5:2-13 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Fikiri kabla ya kusema, wala usiwe mwepesi kusema chochote mbele ya Mungu, kwa maana Mungu yuko mbinguni na wewe uko duniani. Kwa hiyo usiseme mengi.

3. Kadiri mtu anavyohangaika zaidi, ndivyo atakavyoota ndoto;sauti ya mpumbavu ni maneno mengi.

4. Ukimwekea Mungu nadhiri, usikawie kuitimiza; na Mungu hapendezwi na wapumbavu. Tekeleza ulichoahidi.

5. Ni afadhali kutoweka nadhiri kuliko kuweka nadhiri kisha usiitimize.

6. Angalia mdomo wako usikuingize dhambini, halafu ikupase kumwambia mjumbe wa Mungu kwamba hukunuia kutenda dhambi. Ya nini kumfanya Mungu akukasirikie na kuiharibu kazi yako?

7. Ndoto zikizidi, kuna maangamizi na maneno huwa mengi. Jambo la maana ni kumcha Mungu.

8. Usishangae ukiona katika nchi watu fukara wanakandamizwa, wananyimwa haki zao na maslahi yao. Kila mwenye cheo anayewadhulumu wanyonge yupo chini ya mkuu mwingine, na juu ya hao wote kuna wakuu zaidi.

9. Hata hivyo, mfalme akijishughulisha na kilimo ni manufaa kwa wananchi wote.

10. Apendaye fedha hatatosheka na fedha; wala atamaniye mali hata akiipata hatatosheka. Hilo nalo ni bure kabisa.

11. Ongezeko la mali huleta ongezeko la walaji, naye mwenye mali yamfaa nini isipokuwa kuitazama tu mali yake?

12. Usingizi wa kibarua ni mtamu, awe ameshiba au amekula kidogo tu. Lakini usingizi wa tajiri ni wa wasiwasi daima, maana ziada ya mali yake humsumbua usiku kucha.

13. Tena, nimeona jambo moja ovu sana duniani: Mtu alijirundikia mali ikawa hatari kwake.

Kusoma sura kamili Mhubiri 5