Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 7:11-22 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Lakini, Farao akawaita wenye hekima wake na wachawi; hao wachawi wa Misri wakafanya vivyo hivyo kwa uchawi wao.

12. Kila mmoja akaitupa fimbo yake chini, ikawa nyoka. Lakini fimbo ya Aroni ikazimeza fimbo zao.

13. Hata hivyo, moyo wa Farao bado ulibaki kuwa mgumu, wala hakuwasikiliza; ikawa kama alivyosema Mwenyezi-Mungu.

14. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Moyo wa Farao umekuwa mgumu. Anakataa kuwaacha Waisraeli waondoke.

15. Basi, nenda ukakutane naye kesho asubuhi, wakati anapokwenda mtoni Nili. Mngojee kando ya mto. Chukua mkononi mwako ile fimbo iliyogeuka kuwa nyoka.

16. Kisha mwambie hivi, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Waebrania, amenituma kwako, naye asema hivi, ‘Waache watu wangu waende zao ili wanitumikie jangwani, lakini mpaka sasa wewe hupendi kutii.

17. Basi, Mwenyezi-Mungu asema kwamba sasa utamtambua yeye ni nani. Nitayapiga maji ya mto Nili kwa fimbo hii, na maji yote yatageuka kuwa damu.

18. Samaki waliomo mtoni Nili watakufa, mto wote utanuka vibaya, na Wamisri watachukia kabisa kunywa maji yake.’”

19. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mwambie Aroni aichukue fimbo yake na kuinyosha juu ya maji ya Misri, juu ya mito yote, mifereji, madimbwi na mabwawa yao yote, nayo yatakuwa damu. Kutakuwa na damu nchini kote, na hata katika vyombo vyote vya mbao na vya mawe.”

20. Mose na Aroni wakafanya kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru. Aroni aliinua fimbo yake juu mbele ya Farao na maofisa wake, akayapiga maji ya mto Nili, na maji yote mtoni yakageuka kuwa damu.

21. Samaki wakafa, mto ukanuka vibaya sana hata Wamisri wasiweze kunywa maji yake. Nchi nzima ikajaa damu.

22. Lakini wachawi wa Misri kwa kutumia uchawi wao wakafanya vivyo hivyo. Kwa hiyo moyo wa Farao ukabaki kuwa mgumu, naye hakuwasikiliza Mose na Aroni; ikawa kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa amesema.

Kusoma sura kamili Kutoka 7