Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 6:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Lakini Mwenyezi-Mungu akamjibu Mose, “Sasa utaona jinsi nitakavyomtenda Farao; maana kwa nguvu atalazimika kuwaacha watu wangu watoke. Naam, kwa nguvu atawafukuza waondoke nchini mwake.”

2. Mungu akamwambia Mose, “Mimi ni Mwenyezi-Mungu.

3. Nilimtokea Abrahamu, Isaka na Yakobo nikijulikana kama Mungu Mwenye Nguvu, ingawa kwa jina langu, Mwenyezi-Mungu, sikuwajulisha.

4. Tena nilifanya agano nao kwamba nitawapa nchi ya Kanaani ambako waliishi kama wageni.

5. Zaidi ya hayo, nimesikia kilio cha Waisraeli ambao wamelazimishwa kufanya kazi za kitumwa na Wamisri, nikalikumbuka agano langu.

6. Kwa hiyo, waambie Waisraeli hivi, ‘Mimi ni Mwenyezi-Mungu! Mimi nitawatoa katika nira mlizowekewa na Wamisri. Nitawaokoeni utumwani mwenu. Nitaunyosha mkono wangu wenye nguvu na kuwaadhibu vikali Wamisri na kuwakomboa nyinyi.

7. Nitawafanyeni kuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu. Nyinyi mtatambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa katika nira za Wamisri.

8. Nami nitawapeleka katika nchi ile niliyoapa kumpa Abrahamu, Isaka na Yakobo. Nitawapeni nchi hiyo iwe yenu. Mimi ni Mwenyezi-Mungu.’”

9. Mose akawaeleza Waisraeli maneno hayo. Lakini wao hawakumsikiliza kwa sababu walikuwa wamekufa moyo kutokana na utumwa mkali.

10. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,

11. “Nenda kwa Farao, mfalme wa Misri, umwambie awaache Waisraeli waondoke nchini mwake.”

Kusoma sura kamili Kutoka 6