Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 3:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Siku moja, Mose alikuwa anachunga kundi la kondoo la baba mkwe wake, Yethro, kuhani wa Midiani. Mose alilipeleka kundi hilo upande wa magharibi wa jangwa, akaufikia mlima Horebu, mlima wa Mungu.

2. Basi, malaika wa Mwenyezi-Mungu akamtokea katika mwali wa moto katikati ya kichaka. Mose akaangalia, akashangaa kuona kichaka kinawaka moto na wala hakiungui.

3. Basi, akajisemea, “Hiki ni kioja! Kichaka kuwaka moto na kisiungue? Hebu nitazame vizuri.”

4. Mwenyezi-Mungu alipoona kwamba Mose amegeuka kukiangalia kichaka, akamwita pale kichakani, “Mose! Mose!” Mose akaitika, “Naam! Nasikiliza!”

5. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Usije karibu! Vua viatu vyako kwa sababu mahali unaposimama ni mahali patakatifu.”

6. Kisha Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako; Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo.” Mose akaufunika uso wake kwa kuwa aliogopa kumwangalia Mungu.

7. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Nimeyaona mateso ya watu wangu walioko nchini Misri na nimekisikia kilio chao kinachosababishwa na wanyapara wao. Najua mateso yao,

8. na hivyo, nimeshuka ili niwaokoe mikononi mwa Wamisri. Nitawatoa humo nchini na kuwapeleka katika nchi nzuri na kubwa; nchi inayotiririka maziwa na asali, nchi ya Wakanaani, Wahiti, Waamori, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.

9. Naam, kilio cha Waisraeli kimenifikia; nimeona jinsi Wamisri wanavyowatesa.

10. Sasa, nitakutuma kwa Farao ili uwatoe watu wangu, watu hao wa Israeli, kutoka nchini Misri.”

Kusoma sura kamili Kutoka 3