Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 29:22-32 Biblia Habari Njema (BHN)

22. “Kisha utachukua mafuta ya huyo kondoo dume: Mkia wake, mafuta yanayofunika matumbo na sehemu bora ya maini, figo zake mbili na mafuta yake, pamoja na paja la kulia. (Kondoo huyo ni kondoo wa kuweka wakfu.)

23. Kutoka katika kile kikapu cha mikate isiyotiwa chachu kilicho mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu, utachukua mkate mmoja na andazi moja lililotiwa mafuta na mkate mwembamba mmoja.

24. Vyote hivi utamkabidhi Aroni na wanawe nao wataviinua juu kuwa ishara ya kunitolea tambiko mimi Mwenyezi-Mungu.

25. Kisha utavichukua tena kutoka mikononi mwao na kuviteketeza juu ya madhabahu pamoja na ile sadaka ya kuteketezwa, viwe harufu nzuri itakayonipendeza mimi Mwenyezi-Mungu. Hiyo ni sadaka inayotolewa kwa moto.

26. “Kisha utachukua kidari cha huyo kondoo wa kumweka wakfu Aroni, na kufanya ishara ya kunitolea mimi Mwenyezi-Mungu. Nacho kitakuwa sehemu yako.

27. Kuhani anapowekwa wakfu, kidari na paja la kondoo dume wa kuwekea wakfu vitaletwa na kuwekwa wakfu mbele yangu kwa kufanya ishara ya kunitolea, navyo vitakuwa vya Aroni na wanawe.

28. Hivyo Waisraeli daima watachukua sehemu hizo kutoka katika sadaka zao za amani wanazonitolea mimi Mwenyezi-Mungu na kumpa Aroni na wanawe. Hiyo ni sadaka yao kwa Mwenyezi-Mungu.

29. “Baada ya kufa kwake Aroni, mavazi yake matakatifu yatakabidhiwa wazawa wake, nao watayavaa siku yao ya kupakwa mafuta na kuwekewa mikono.

30. Mwana wa Aroni atakayekuwa kuhani mahali pa baba yake atayavaa mavazi hayo siku saba katika hema la mkutano, ili kuhudumu katika mahali patakatifu.

31. “Utachukua nyama ya huyo kondoo wa kuwaweka wakfu na kuichemshia katika mahali patakatifu.

32. Kisha utawapa Aroni na wanawe, nao wataila mlangoni pa hema la mkutano pamoja na ile mikate iliyosalia kapuni.

Kusoma sura kamili Kutoka 29