Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 28:24-40 Biblia Habari Njema (BHN)

24. na mikufu miwili ya dhahabu uifunge kwenye pete hizo za kifuko cha kifuani.

25. Zile ncha mbili za mkufu wa dhahabu utazishikamanisha kwenye vile vijalizo viwili vya kile kibati ili zishikamane na kipande cha mabegani cha kizibao upande wa mbele.

26. Pia utatengeneza pete mbili za dhahabu na kuzitia kwenye ncha mbili za chini upande wa ndani wa kifuko cha kifuani karibu na kizibao.

27. Kisha utatengeneza pete nyingine mbili za dhahabu na kuzitia mbele katika ncha za chini za vipande vya kizibao, mahali kizibao kinapoungana na mkanda uliofumwa kwa ustadi.

28. Kifuko cha kifuani kitafungwa kwenye kizibao kwa kufunganisha pete zake na kizibao kwa kamba ya rangi ya buluu, ili kifuko hicho cha kifuani kisilegee ila kikalie ule mkanda uliofumwa kwa ustadi.

29. “Aroni anapoingia mahali patakatifu, atavaa kifuko cha kauli kimechorwa majina ya makabila ya wana wa Israeli; kwa namna hiyo mimi Mwenyezi-Mungu sitawasahau nyinyi kamwe.

30. Kwenye kifuko hicho utatia mawe ya kauli yaninginie kifuani mwa Aroni kila anapokuja mbele yangu. Nyakati hizo ni lazima kila mara kuvaa kifuko hicho, ili aweze kutambua matakwa yangu kuhusu Waisraeli.

31. “Utashona kanzu ya kuvalia kizibao kwa sufu ya rangi ya buluu.

32. Itakuwa na nafasi ya kupitishia kichwa katikati, na nafasi hiyo itazungushiwa utepe uliofumwa ili isichanike.

33. Kwenye upindo wake wa chini, kuzunguka pande zote, itapambwa kwa makomamanga ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, kutakuwa pia na njuga za dhahabu kati ya hayo makomamanga:

34. Komamanga, njuga, komamanga, njuga, kuizunguka kanzu yote.

35. Aroni atavaa kanzu hiyo kutekeleza huduma yake ya ukuhani na sauti yake itasikika wakati anapoingia mahali patakatifu mbele yangu na wakati anapotoka, njuga hizo zitasikika, naye hatauawa.

36. “Kisha, utatengeneza kibati cha dhahabu safi na kuchora juu yake kama mtu achoravyo mhuri, ‘Wakfu kwa Mwenyezi-Mungu.’

37. Kibati hicho utakifunga mbele ya kilemba kwa ukanda wa buluu.

38. Aroni atakivaa kibati hicho kwenye paji la uso wake; kwa hicho kibati atachukua lawama ya makosa ambayo Waisraeli wanaweza kuwa wameyafanya katika kunitolea tambiko takatifu, nami nitazikubali tambiko zao.

39. Utamtengenezea Aroni joho iliyonakshiwa kwa kitani safi na kumfumia kilemba cha kitani safi na ukanda ulionakshiwa vizuri.

40. “Utawatengenezea wana wa Aroni majoho, mishipi na kofia ili waonekane wana utukufu na uzuri.

Kusoma sura kamili Kutoka 28