Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 23:9-21 Biblia Habari Njema (BHN)

9. “Usimdhulumu mgeni; nyinyi mwajua hali ya kuwa mgeni, maana mlikuwa wageni nchini Misri.

10. “Kwa muda wa miaka sita utapanda mashamba yako na kuvuna mazao yake.

11. Lakini mnamo mwaka wa saba, utayaacha mashamba yako bila kupanda mbegu, ili maskini miongoni mwa watu wako wapate chakula kilichosalia humo, na wanyama wa porini wale. Utafanya vivyo hivyo katika shamba lako la mizabibu na la mizeituni.

12. “Kwa siku sita utafanya kazi zako, lakini siku ya saba utapumzika, ili ng'ombe wako na punda wako pia wapate kupumzika; na watumwa wako na watumishi wa kigeni wapate kustarehe.

13. Yazingatie yote niliyokuambia. Usiyataje hata kidogo majina ya miungu mingine; hayo yasisikike kinywani mwako.

14. “Mara tatu kila mwaka mtafanya sikukuu kwa heshima yangu.

15. Mtaadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu: Kama nilivyowaagiza, mtakula mikate isiyotiwa chachu kwa siku saba wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu, kwa sababu katika mwezi huo mlitoka Misri. Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu.

16. Mtaadhimisha sikukuu ya mavuno ya kwanza ya kazi zenu na ya mavuno ya mashamba yenu. Mtaadhimisha sikukuu ya kukusanya mavuno mwishoni mwa mwaka mnapokusanya mazao ya kazi zenu.

17. Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakusanyika mbele zangu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu.

18. “Usinitolee damu ya tambiko yangu pamoja na mkate uliotiwa chachu, wala usiyaache mafuta ya sikukuu yangu yabaki mpaka asubuhi.

19. “Mazao ya kwanza ya ardhi yako utayaleta nyumbani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.“Usimchemshe mwanakondoo au mwanambuzi katika maziwa ya mama yake.

20. “Tazameni, mimi namtuma malaika awatangulie safarini ili awalinde na kuwafikisha katika nchi niliyowatayarishia.

21. Msikilizeni na kutii atakachosema, wala msimwasi, kwani hatawasamehe uasi wenu maana nimemtuma kwa jina langu.

Kusoma sura kamili Kutoka 23