Sura

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
  17. 17
  18. 18
  19. 19
  20. 20
  21. 21
  22. 22
  23. 23
  24. 24
  25. 25
  26. 26
  27. 27
  28. 28
  29. 29
  30. 30
  31. 31
  32. 32
  33. 33
  34. 34
  35. 35
  36. 36
  37. 37
  38. 38
  39. 39
  40. 40

Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 23 Biblia Habari Njema (BHN)

Haki na usawa

1. “Usitoe habari za uongo. Usishirikiane na mtu mwovu ili kuwa shahidi mbaya.

2. Usifuate genge la watu kutenda uovu, wala usijumuike na genge la watu kutoa ushahidi mahakamani ili kupotosha haki.

3. Usiwe na upendeleo katika kesi ya maskini.

4. “Ukimkuta ng'ombe au punda wa adui yako amepotea, utamrudishia mwenyewe.

5. Ukimwona punda wa mtu anayekuchukia ameanguka na mzigo wake, msaidie mtu huyo kumsimamisha punda wake, wala usimwache na kwenda zako.

6. “Usiipotoshe haki anayostahili maskini katika kesi yake.

7. Jitenge mbali na mashtaka ya uongo wala usiwaue wasio na hatia na waadilifu, maana mimi sitamsamehe mtu mwovu.

8. Usipokee rushwa, maana rushwa huwapofusha wakuu na kupotosha mambo ya wenye haki.

9. “Usimdhulumu mgeni; nyinyi mwajua hali ya kuwa mgeni, maana mlikuwa wageni nchini Misri.

Mwaka wa saba

10. “Kwa muda wa miaka sita utapanda mashamba yako na kuvuna mazao yake.

11. Lakini mnamo mwaka wa saba, utayaacha mashamba yako bila kupanda mbegu, ili maskini miongoni mwa watu wako wapate chakula kilichosalia humo, na wanyama wa porini wale. Utafanya vivyo hivyo katika shamba lako la mizabibu na la mizeituni.

12. “Kwa siku sita utafanya kazi zako, lakini siku ya saba utapumzika, ili ng'ombe wako na punda wako pia wapate kupumzika; na watumwa wako na watumishi wa kigeni wapate kustarehe.

13. Yazingatie yote niliyokuambia. Usiyataje hata kidogo majina ya miungu mingine; hayo yasisikike kinywani mwako.

Sikukuu tatu kubwa

14. “Mara tatu kila mwaka mtafanya sikukuu kwa heshima yangu.

15. Mtaadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu: Kama nilivyowaagiza, mtakula mikate isiyotiwa chachu kwa siku saba wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu, kwa sababu katika mwezi huo mlitoka Misri. Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu.

16. Mtaadhimisha sikukuu ya mavuno ya kwanza ya kazi zenu na ya mavuno ya mashamba yenu. Mtaadhimisha sikukuu ya kukusanya mavuno mwishoni mwa mwaka mnapokusanya mazao ya kazi zenu.

17. Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakusanyika mbele zangu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu.

18. “Usinitolee damu ya tambiko yangu pamoja na mkate uliotiwa chachu, wala usiyaache mafuta ya sikukuu yangu yabaki mpaka asubuhi.

19. “Mazao ya kwanza ya ardhi yako utayaleta nyumbani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.“Usimchemshe mwanakondoo au mwanambuzi katika maziwa ya mama yake.

Ahadi na maagizo

20. “Tazameni, mimi namtuma malaika awatangulie safarini ili awalinde na kuwafikisha katika nchi niliyowatayarishia.

21. Msikilizeni na kutii atakachosema, wala msimwasi, kwani hatawasamehe uasi wenu maana nimemtuma kwa jina langu.

22. Lakini mkimsikiliza kwa makini na kufanya yote asemayo, mimi nitakuwa adui wa adui zenu na mpinzani wa wapinzani wenu.

23. Malaika wangu atakapowaongoza na kuwafikisha katika nchi ya Waamori, Wahiti, Waperizi, Wakanaani, Wahivi na Wayebusi, nami nikawaangamiza hao wote,

24. msiiname mbele ya miungu yao kuiabudu, wala kuitumikia, wala msiige mambo yao. Bali mtawaangamiza kabisa na kuzivunjavunja nguzo zao.

25. Mtanitumikia mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nami nitawabariki kwa chakula na maji na kuyaondoa magonjwa kati yenu.

26. Hakutakuwa na mwanamke yeyote atakayepoteza mimba wala kuwa tasa katika nchi yenu. Nami nitawajalia maisha marefu.

27. “Nitapeleka kitisho mbele yenu na kuwavuruga watu wote mtakaowakabili, na adui zenu nitawafanya wageuke na kuwakimbia.

28. Nitapeleka manyigu mbele yenu ambao watawafukuza Wahivi, Wakanaani na Wahiti.

29. Sitawaondoa watu hao katika mwaka mmoja, nchi isije ikabaki tupu na wanyama wa porini wakaongezeka mno na kuwazidi nguvu.

30. Lakini nitawaondoa kidogokidogo mpaka hapo mtakapoongezeka na kuimiliki nchi hiyo.

31. Mipaka ya nchi yenu itakuwa kutoka bahari ya Shamu hadi bahari ya Mediteranea, na kutoka jangwani mpaka mto Eufrate, maana nitawatia wakazi wa nchi hiyo mikononi mwenu, nanyi mtawafukuza wawaondoke.

32. Msifanye agano lolote nao, wala na miungu yao.

33. Msiwaruhusu waishi nchini mwenu wasije wakawafanya mtende dhambi dhidi yangu; maana kama mkiitumikia miungu yao, hakika hiyo itakuwa mtego wa kuwanasa.”