Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 23:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. “Usitoe habari za uongo. Usishirikiane na mtu mwovu ili kuwa shahidi mbaya.

2. Usifuate genge la watu kutenda uovu, wala usijumuike na genge la watu kutoa ushahidi mahakamani ili kupotosha haki.

3. Usiwe na upendeleo katika kesi ya maskini.

4. “Ukimkuta ng'ombe au punda wa adui yako amepotea, utamrudishia mwenyewe.

5. Ukimwona punda wa mtu anayekuchukia ameanguka na mzigo wake, msaidie mtu huyo kumsimamisha punda wake, wala usimwache na kwenda zako.

6. “Usiipotoshe haki anayostahili maskini katika kesi yake.

7. Jitenge mbali na mashtaka ya uongo wala usiwaue wasio na hatia na waadilifu, maana mimi sitamsamehe mtu mwovu.

8. Usipokee rushwa, maana rushwa huwapofusha wakuu na kupotosha mambo ya wenye haki.

9. “Usimdhulumu mgeni; nyinyi mwajua hali ya kuwa mgeni, maana mlikuwa wageni nchini Misri.

10. “Kwa muda wa miaka sita utapanda mashamba yako na kuvuna mazao yake.

11. Lakini mnamo mwaka wa saba, utayaacha mashamba yako bila kupanda mbegu, ili maskini miongoni mwa watu wako wapate chakula kilichosalia humo, na wanyama wa porini wale. Utafanya vivyo hivyo katika shamba lako la mizabibu na la mizeituni.

12. “Kwa siku sita utafanya kazi zako, lakini siku ya saba utapumzika, ili ng'ombe wako na punda wako pia wapate kupumzika; na watumwa wako na watumishi wa kigeni wapate kustarehe.

13. Yazingatie yote niliyokuambia. Usiyataje hata kidogo majina ya miungu mingine; hayo yasisikike kinywani mwako.

Kusoma sura kamili Kutoka 23