Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 18:5-17 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Yethro, mkwewe Mose, alikuja pamoja na binti yake, yaani mkewe Mose, pamoja na watoto, akamkuta Mose jangwani alikokuwa amepiga kambi kwenye mlima wa Mungu.

6. Mose alipoambiwa kuwa baba mkwe wake pamoja na mkewe na wanawe wawili wanakuja,

7. alitoka kwenda kumlaki baba mkwe wake, akamwinamia na kumbusu. Wakasalimiana, kisha wakaingia hemani.

8. Mose akamweleza mkwewe mambo yote Mwenyezi-Mungu aliyomtenda Farao na Wamisri kwa ajili ya Waisraeli. Alimwambia pia juu ya shida zote zilizowapata safarini na jinsi Mwenyezi-Mungu alivyowaokoa.

9. Yethro akafurahishwa na yote aliyotenda Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya Waisraeli, kwa kuwaokoa mikononi mwa Wamisri.

10. Yethro akasema, “Na atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye amewaokoa mikononi mwa Wamisri na kutoka utumwa wa Farao.

11. Sasa najua kwamba Mwenyezi-Mungu ni mkuu kuliko miungu yote, kwani amewakomboa watu hawa mikononi mwa Wamisri ambao waliwatendea ujeuri.”

12. Hapo Yethro, baba mkwe wa Mose, akamtolea Mungu sadaka za kuteketezwa na tambiko. Naye Aroni akaja pamoja na wazee wa Israeli ili kula chakula pamoja na Yethro, mbele ya Mwenyezi-Mungu.

13. Kesho yake, Mose aliketi kuamua matatizo ya Waisraeli, nao wakasimama wakiwa wamemzunguka, tangu asubuhi mpaka jioni.

14. Yethro, baba mkwe wa Mose, alipoyaona mambo yote ambayo Mose aliwafanyia Waisraeli, alimwuliza, “Kwa nini unawafanyia watu mambo haya? Mbona unaketi peke yako huku watu wamekuzunguka tangu asubuhi mpaka jioni?”

15. Mose akamjibu mkwewe, “Kwa sababu watu huja kwangu kuuliza matakwa ya Mungu.

16. Wakiwa na ugomvi wowote ule wao huja kwangu nami huamua kati ya mtu na mwenzake, na kuwafunza amri za Mungu na maamuzi yake.”

17. Basi, Yethro akamwambia Mose, “Unavyofanya si vizuri!

Kusoma sura kamili Kutoka 18