Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 16:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Jumuiya yote ya Waisraeli iliondoka, ikafika jangwa la Sini kati ya Elimu na Sinai. Hii ilikuwa siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili tangu walipoondoka nchini Misri.

2. Basi, jumuiya yote ya Waisraeli ikawalalamikia Mose na Aroni huko jangwani,

3. “Laiti Mwenyezi-Mungu angelituua tulipokuwa nchini Misri ambako tulikaa, tukala nyama na mikate hata tukashiba. Lakini nyinyi mmetuleta huku jangwani kuiua jumuiya hii yote kwa njaa!”

4. Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mimi nitawanyeshea mikate kutoka mbinguni. Kila siku watu watatoka na kukusanya chakula cha siku hiyo. Kwa njia hii nitawajaribu nione kama watazifuata sheria zangu au hawatazifuata.

5. Lakini siku ya sita, wakati watakapoandaa chakula walichokusanya, kiasi hicho kitakuwa mara mbili ya chakula cha kila siku.”

6. Basi, Mose na Aroni wakawaambia watu wote wa Israeli, “Jioni, mtatambua kwamba Mwenyezi-Mungu ndiye aliyewatoa nchini Misri!

7. Tena, kesho asubuhi, mtauona utukufu wa Mwenyezi-Mungu kwani ameyasikia manunguniko mliyomnungunikia. Sisi ni nani hata mtunungunikie?”

8. Tena Mose akasema, “Jioni, Mwenyezi-Mungu atawapeni nyama mle, na asubuhi atawapeni mikate mle mshibe, maana yeye ameyasikia manunguniko mliyomnungunikia. Sisi ni nani hata mtunungunikie? Msitunungunikie sisi bali mnungunikieni Mwenyezi-Mungu.”

9. Kisha Mose akamwambia Aroni, “Iambie jumuiya yote ya Waisraeli ikusanyike mbele ya Mwenyezi-Mungu kwani ameyasikia manunguniko yenu.”

10. Wakati Aroni alipokuwa akizungumza na jumuiya ya Waisraeli, watu wote walitazama huko jangwani, na mara utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukaonekana mawinguni.

11. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,

12. “Nimeyasikia manunguniko ya Waisraeli. Basi, waambie kwamba wakati wa jioni watakula nyama, na asubuhi watakula mkate. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.”

13. Basi, mnamo wakati wa jioni kukaja kware wengi, wakafunika kambi ya Waisraeli. Asubuhi yake kukatokea umande, ukatanda kandokando ya kambi yao.

Kusoma sura kamili Kutoka 16