Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 14:9-18 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Wamisri pamoja na farasi wao wote, magari ya farasi ya vita na wapandafarasi wake waliwafuata Waisraeli, wakawakuta wamepiga kambi kando ya bahari, karibu na Pi-hahirothi, mbele ya Baal-sefoni.

10. Waisraeli walipotazama na kumwona Farao akija na jeshi lake dhidi yao, walishikwa na hofu kubwa, wakamlilia Mwenyezi-Mungu.

11. Wakamwambia Mose, “Je, hapakuwa na makaburi ya kutosha nchini Misri hata ukatuleta tufie huku jangwani? Mbona umetutendea haya, kwa tututoa katika nchi ya Misri?

12. Je, hatukukuambia mambo haya tulipokuwa bado Misri? Tulikuambia utuache tuendelee kuwatumikia Wamisri. Ingalikuwa afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufia huku jangwani.”

13. Mose akawaambia Waisraeli, “Msiogope! Kaeni imara! Leo mtaona jinsi Mwenyezi-Mungu atakavyowaokoa. Maana, hawa Wamisri mnaowaona leo, hamtawaona tena.

14. Mwenyezi-Mungu atawapigania; nyinyi mnachotakiwa kufanya ni kutulia tu.”

15. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kwa nini mnanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele.

16. Inua fimbo yako na kuinyosha juu ya bahari. Maji yatagawanyika na Waisraeli wataweza kuvuka katikati ya bahari mahali pakavu.

17. Mimi nitawafanya Wamisri kuwa wakaidi, nao watawafuatia katikati ya bahari; nami nitajipatia utukufu kutokana na kuangamizwa kwa Farao na jeshi lake, magari yake ya vita pamoja na wapandafarasi wake.

18. Naam, nitatukuka kwa kumwangamiza Farao na jeshi lake, pamoja na magari yake na wapandafarasi; nao Wamisri watajua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.”

Kusoma sura kamili Kutoka 14