Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 13:14-20 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Kama hapo baadaye mwanao akiuliza maana ya jambo hili, utamwambia, ‘Kwa nguvu ya mkono wake, Mwenyezi-Mungu alitutoa nchini Misri ambako tulikuwa watumwa.

15. Farao kwa ukaidi alikataa kutuachia tuondoke; kwa hiyo Mwenyezi-Mungu alimuua kila mzaliwa wa kwanza nchini Misri, mzaliwa wa kwanza wa binadamu na wa mnyama. Basi, mimi ninamtolea sadaka Mwenyezi-Mungu kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa mifugo yangu, lakini kila mzaliwa wa kwanza wa wanangu namkomboa.’

16. Jambo hili litakuwa kama alama mkononi mwako au utepe katika paji la uso wako, kwamba Mwenyezi-Mungu alitutoa nchini Misri kwa mkono wenye nguvu.”

17. Wakati Farao alipowaachia Waisraeli waende zao, Mungu hakuwapitisha katika nchi ya Wafilisti, ingawa njia hiyo ilikuwa ya karibu. Mungu alisema, “Sipendi watu hawa wabadilishe nia na kurudi Misri wakijua itawabidi kupigana vita.”

18. Badala yake, Mungu aliwapitisha Waisraeli katika njia ya mzunguko kupitia jangwani, kuelekea bahari ya Shamu. Waisraeli waliondoka nchini Misri wakiwa wamejiandaa kwa vita.

19. Mose aliichukua mifupa ya Yosefu kama Yosefu alivyoagiza kabla ya kufa kwake. Alikuwa amewaapisha rasmi Waisraeli akisema, “Mungu atakapowajia kuwatoa nchini humu, ni lazima mwichukue mifupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi.”

20. Basi, Waisraeli waliondoka Sukothi, wakapiga kambi huko Ethamu, ukingoni mwa jangwa.

Kusoma sura kamili Kutoka 13