Agano la Kale

Agano Jipya

Kumbukumbu La Sheria 9:13-27 Biblia Habari Njema (BHN)

13. “Kadhalika, Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Nimewaona watu hawa, ni watu wakaidi sana;

14. niache niwaangamize, nilifutilie mbali jina lao duniani; nami nitakufanya wewe kuwa taifa lenye nguvu na kubwa kuliko wao.’

15. “Basi, niligeuka, nikashuka kutoka mlimani, nikiwa nimebeba vile vibao viwili vya mawe, nao moto ulikuwa unawaka mlimani.

16. Nilitazama, nikaona kwamba tayari mmekwisha kutenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; mlikwisha jitengenezea sanamu ya ndama ya kusubu; bila kukawia mlikwisha iacha njia ya Mwenyezi-Mungu ambayo aliwaamuru.

17. Hivyo, nilivishika vile vibao viwili nikavitupa chini, nikavivunja mbele yenu.

18. Kisha nikalala chini kifudifudi mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama hapo awali, kwa muda wa siku arubaini usiku na mchana; sikula chakula wala kunywa maji, kwa sababu ya dhambi mliyokuwa mmetenda kwa kufanya maovu mbele yake Mwenyezi-Mungu kwa kumkasirisha.

19. Niliogopa kwamba hasira na ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu dhidi yenu, ingewaangamiza; lakini Mwenyezi-Mungu alinisikiliza pia wakati huo.

20. Hali kadhalika, Mwenyezi-Mungu alikuwa amemkasirikia sana Aroni, kiasi cha kumwangamiza; hivyo, nikamwombea Aroni wakati huohuo.

21. Kile kitu kiovu, yaani yule ndama mliyejitengenezea, nilikichukua, nikakiteketeza motoni, nikakipondaponda na kukisagasaga, kikawa mavumbi laini; halafu nikayatupa hayo mavumbi kwenye kijito kilichotiririka chini ya mlima huo.

22. “Pia mlimkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, huko Tabera, Masa na Kibroth-hataava.

23. Na Mwenyezi-Mungu alipowatuma kutoka Kadesh-barnea akisema, ‘Nendeni mkaimiliki nchi ambayo nimewapatia,’ mlimwasi; hamkusadiki wala hamkutii yale aliyowaambia.

24. Nyinyi mmekuwa waasi dhidi ya Mwenyezi-Mungu tangu siku nilipowajua.

25. “Kwa hiyo, nililala kifudifudi mbele ya Mwenyezi-Mungu siku hizo arubaini, usiku na mchana, kwa sababu Mwenyezi-Mungu alikuwa amesema atawaangamiza.

26. Nilimwomba Mwenyezi-Mungu, nikisema. ‘Ee Mwenyezi-Mungu, usiwaangamize watu wako na urithi wako, watu uliowakomboa na kuwatoa katika nchi ya Misri kwa uwezo na nguvu yako kubwa.

27. Wakumbuke watumishi wako, Abrahamu, Isaka na Yakobo, wala usiujali ukaidi, uovu na dhambi za watu hawa.

Kusoma sura kamili Kumbukumbu La Sheria 9