Agano la Kale

Agano Jipya

Kumbukumbu La Sheria 7:2-20 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Pia, baada ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuyatia mikononi mwenu, mkawashinda watu hao na kuwaangamiza kabisa, msifanye agano lolote nao wala msiwahurumie.

3. Msioane nao, wala msiwaoze binti zenu au wana wenu kwao.

4. Mkifanya hivyo wao watawapotosha watoto wenu wasimfuate Mwenyezi-Mungu, na kuwafanya waabudu miungu mingine, nayo hasira ya Mwenyezi-Mungu itawaka juu yenu, halafu atawaangamiza mara moja.

5. Lakini watendeni hivi: Mtazivunjilia mbali madhabahu zao na kuzibomoa nguzo zao. Na sanamu za Ashera mtazikatilia mbali na kuzitia moto sanamu zao za kuchonga.

6. Fanyeni hivyo kwa kuwa nyinyi mmewekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Kati ya watu wote ulimwenguni aliwachagua nyinyi ili muwe taifa lake mwenyewe.

7. “Mwenyezi-Mungu hakuwapenda nyinyi na kuwateua kwa kuwa nyinyi ni wengi mno kuliko watu wengine; nyinyi mlikuwa wachache kuliko mataifa mengine duniani.

8. Lakini ni kwa sababu Mwenyezi-Mungu anawapenda na anashika kiapo alichowaapia babu zenu, ndiyo maana aliwaokoeni kwa mkono wake wenye nguvu na kuwaokoa toka utumwani, toka mikono ya Farao mfalme wa Misri.

9. Basi, jueni kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye Mungu; ni Mungu mwaminifu, anayeshika agano lake na huwaonesha fadhili kwa vizazi vingi vya wale wanaoshika amri zake.

10. Lakini huwalipa wanavyostahili wale wanaomchukia, wala hatasita kuwaadhibu wanaomchukia.

11. Kwa hiyo muwe waangalifu kushika amri, masharti na maagizo ninayowaamuru leo.

12. “Mkisikiliza maagizo haya na kuyashika hata kuyatenda, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atashika agano lake nanyi na atawaonesheni fadhili kama alivyowaahidi babu zenu.

13. Atawapenda na kuwabariki, nanyi mtaongezeka na kuwa na wazawa wengi; atayabariki mashamba yenu ili mpate nafaka, divai na mafuta; atawabariki kwa kuwapeni ng'ombe na kondoo wengi katika nchi aliyowaahidi babu zenu kuwa atawapeni nyinyi.

14. Mtabarikiwa kuliko watu wengine wote ulimwenguni. Miongoni mwenu hakutakuwa na mwanamume wala mwanamke tasa.

15. Mwenyezi-Mungu atawaondoleeni magonjwa yote na hamtapatwa na magonjwa yoyote ya kutisha kama yaliyowapata huko Misri, lakini atawapa maadui zenu magonjwa hayo.

16. Angamizeni taifa lolote ambalo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; atalitia mikononi mwenu, wala msilionee huruma. Msiabudu miungu yao, kwani jambo hili litakuwa mtego kwenu.

17. “Msijisemee mioyoni mwenu: ‘Watu hawa ni wengi kuliko sisi, twawezaje kuwafukuza nchini?’

18. Msiwaogope, kumbukeni vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyomtendea Farao na nchi nzima ya Misri.

19. Kumbukeni maradhi mabaya mliyoyaona kwa macho yenu, miujiza na maajabu na nguvu kubwa na uwezo mkuu, ambavyo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; alitumia kuwakomboa; hivyo ndivyo atakavyowatenda watu mnaowaogopa.

20. Zaidi ya hayo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atapeleka mavu kati yao na kuwaangamiza wale ambao watawatoroka ili kujificha.

Kusoma sura kamili Kumbukumbu La Sheria 7