Agano la Kale

Agano Jipya

Kumbukumbu La Sheria 16:4-14 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Kwa muda wa siku saba mtu yeyote katika nchi yenu asiweke chachu nyumbani mwake; na nyama ya yule mnyama aliyechinjwa jioni ya siku ya kwanza isibaki mpaka asubuhi.

5. Msitolee sadaka ya Pasaka katika mji wowote ambao Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa,

6. bali mtaitolea pale mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atapachagua likae jina lake, hapo ndipo mtakapotolea sadaka ya Pasaka jioni, jua linapotua, wakati uleule mlipotoka Misri.

7. Hiyo nyama mtaichemsha na kuila mahali pale Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atakapochagua; asubuhi yake mtageuka na kurudi mahemani mwenu.

8. Kwa siku sita mtakula mikate isiyotiwa chachu; na mnamo siku ya saba utakuwapo mkutano mkubwa wa kumwabudu Mwenyezi-Mungu, na msifanye kazi yoyote siku hiyo.

9. “Mtahesabu majuma saba; mtaanza kuyahesabu tangu mnapoanza kuvuna nafaka.

10. Halafu mtaadhimisha sikukuu ya majuma kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kutoa sadaka ya hiari, mtakayotoa kadiri awabarikiavyo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

11. Mtafurahia mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nyinyi pamoja na wana wenu na binti zenu, watumishi wenu, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao wanaishi pamoja nanyi. Fanyeni haya katika mahali Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atakapochagua likae jina lake.

12. Mkumbuke kuwa mlikuwa watumwa kule Misri; basi muwe waangalifu kufuata masharti haya.

13. “Baada ya kupura nafaka yenu yote na kukamua zabibu zenu, adhimisheni sikukuu ya vibanda kwa muda wa siku saba.

14. Mtafanya sherehe hiyo, nyinyi na watoto wenu wa kiume na wa kike, watumishi wenu, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao huishi katika miji yenu.

Kusoma sura kamili Kumbukumbu La Sheria 16