Agano la Kale

Agano Jipya

Kumbukumbu La Sheria 10:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. “Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia, ‘Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, na sanduku la mbao, halafu uje kwangu huku juu mlimani,

2. nami nitaandika maneno yaliyokuwa yameandikwa katika vibao vile ulivyovunja, kisha viweke vibao hivyo katika sanduku’.

3. “Basi, nikatengeneza sanduku la mshita na vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, nikavitwaa mkononi, nikapanda navyo mlimani.

4. Mwenyezi-Mungu akaandika katika vibao hivyo maneno yaleyale kama ya hapo awali: Amri kumi ambazo aliwapeni alipoongea kutoka katika moto siku ya mkutano. Halafu Mwenyezi-Mungu akanipa vibao hivyo.

5. Niligeuka, nikashuka kutoka mlimani, na kama Mwenyezi-Mungu alivyoniagiza, niliviweka vibao hivyo ndani ya sanduku nililokuwa nimelitengeneza, na vimo ndani ya sanduku hilo, kama Mwenyezi-Mungu alivyoniamuru.”

6. (Watu wa Israeli walisafiri kutoka visima vya watu wa Yaakani hadi Mosera. Hapo, Aroni alifariki, akazikwa. Eleazari mwanawe, akachukua nafasi yake kama kuhani.

7. Kutoka hapo, walisafiri hadi Gudgoda, na kutoka Gudgoda hadi Yot-batha, eneo lenye vijito vingi vya maji.

8. Wakati huo, Mwenyezi-Mungu aliwateua watu wa kabila la Lawi wawe wakilibeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, wamtumikie kama makuhani na kubariki watu kwa jina lake hata hivi leo.

9. Ndio maana kabila la watu wa Lawi halina sehemu ya nchi ya urithi pamoja na ndugu zao; walichopokea ni heshima ya kuwa makuhani wa Mwenyezi-Mungu, kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyoahidi).

10. “Nilikaa mlimani kwa muda wa siku arubaini, usiku na mchana, kama hapo awali. Mwenyezi-Mungu alinisikiliza kwa mara nyingine tena na akakubali kwamba hatawaangamiza.

11. Kisha akaniambia ‘Ondoka uendelee na safari yako ukiwaongoza watu ili waweze kuingia na kuimiliki nchi niliyowaapia babu zenu ya kuwa nitawapa’.

Kusoma sura kamili Kumbukumbu La Sheria 10