Agano la Kale

Agano Jipya

Isaya 60:11-22 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Malango yako yatakuwa wazi daima;usiku na mchana hayatafungwa,ili watu wakuletee utajiri wa mataifa,pamoja na wafalme wao katika maandamano.

12. Kila ufalme au taifa lisilokutumikia litaangamia;mataifa hayo yatatokomezwa kabisa.

13. “Utaletewa fahari ya msitu wa Lebanoni:Mbao za miberoshi, mivinje na misonobari,zitumike kupamba mahali pa maskani yangu;nami nitaparembesha hapo ninapokaa.

14. Wazawa wa wale waliokudhulumu,watakuja na kukuinamia kwa heshima.Wote wale waliokudharau,watasujudu mbele ya miguu yako.Watakuita: ‘Mji wa Mwenyezi-Mungu’,‘Siyoni, Mji wa Mtakatifu wa Israeli’.

15. “Wewe ulikuwa umeachwa na kuchukiwa,hakuna aliyependa hata kupitia kwako.Lakini sasa nitakufanya uwe na fahari milele,utakuwa mji wa furaha kizazi hata kizazi.

16. Utaletewa chakula na watu wa mataifa,naam, wafalme watakupatia chakula bora.Hapo utatambua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ni Mwokozi wako;mimi Mwenye Nguvu wa Yakobo ni Mkombozi wako.

17. “Badala ya shaba nitakuletea dhahabu,badala ya chuma nitakuletea fedha,badala ya miti, nitakuletea shaba,na badala ya mawe nitakuletea chuma.Amani itatawala juu yako,uadilifu utakuongoza.

18. Ukatili hautasikika tena nchini mwako;wala uharibifu na maangamizi ndani ya mipaka yako.Utaweza kuziita kuta zako: ‘Wokovu’,na malango yako: ‘Sifa’.

19. “Hutahitaji tena jua kukuangazia mchana,wala mwezi kukumulikia usiku;maana mimi Mwenyezi-Mungu ni mwanga wako milele;mimi Mungu wako nitakuwa fahari yako.

20. Mwanga wako mchana hautatua kama jua,wala mwangaza wako usiku kufifia kama mbalamwezi;maana Mwenyezi-Mungu ni mwanga wako milele,nazo siku zako za kuomboleza zitakoma.

21. Watu wako wote watakuwa waadilifu,nao wataimiliki nchi milele.Hao ni chipukizi nililopanda mimi,kazi ya mikono yangu kwa ajili ya utukufu wangu.

22. Aliye mdogo kati yenu atakuwa ukoo,aliye mdogo kuliko wote atakuwa taifa kubwa.Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu;wakati ufikapo nitayatekeleza hayo haraka.”

Kusoma sura kamili Isaya 60