Agano la Kale

Agano Jipya

Isaya 41:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mungu asema hivi:“Enyi wakazi wa mbali nyamazeni mnisikilize!Enyi mataifa jipeni nguvu;jitokezeni mkatoe hoja zenu,na tuje pamoja kwa hukumu.

2. “Nani, ila mimi, aliyemwita shujaa toka mashariki,mtu ambaye hupata ushindi popote aendako?Mimi huyatia mataifa makuchani mwake,naye huwaponda wafalme chini ya miguu yake!Upanga wake huwafanya kuwa kama vumbi,kwa upinde wake huwapeperusha kama makapi.

3. Yeye huwafuatia na kupita salama;huenda kasi kana kwamba hagusi chini.

4. Nani aliyefanya yote haya yatendeke?Ni nani aliyepanga wakati wa kila tukio?Mimi Mwenyezi-Mungu nipo tangu mwanzo,mimi nitakuwapo hata milele.

5. “Wakazi wa mbali wameona niliyotenda, wakaogopa;dunia yote inatetemeka kwa hofu.Watu wote wamekusanyika, wakaja.

6. Kila mmoja anamhimiza mwenzake akisema,‘Haya! Jipe moyo!’

7. Fundi anamhimiza mfua dhahabu,naye alainishaye sanamu kwa nyundo,anamhimiza anayeiunga kwa misumari.Wote wanasema, ‘Imeungika vizuri sana!’Kisha wanaifunga kwa misumari isitikisike.

8. “Sikiliza ewe Israeli, mtumishi wangu,wewe, Yakobo ambaye nimekuchagua,wewe mzawa wa Abrahamu, rafiki yangu;

9. wewe niliyekuleta toka miisho ya dunia,wewe niliyekuambia: ‘Wewe u mtumishi wangu;mimi sikukutupa, bali nilikuchagua.’

10. Basi, usiogope, mimi nipo pamoja nawe.Usifadhaike, mimi ni Mungu wako.Nitakuimarisha na kukusaidia;nitakulinda kwa mkono wangu wa ushindi.

11. “Naam! Wote waliokuwakia hasira,wataaibishwa na kupata fedheha.Wote wanaopingana nawe,watakuwa si kitu na kuangamia.

12. Utawatafuta hao wanaopingana nawe,lakini watakuwa wameangamia.

13. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako,ndimi ninayetegemeza mkono wako.Mimi ndimi ninayekuambia:‘Usiogope, nitakusaidia.’”

14. Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Enyi watu wa Yakobo dhaifu kama mdudu,enyi Waisraeli, msiogope!Mimi Mwenyezi-Mungu nasema nitawasaidia.Mimi ni Mkombozi wenu,Mtakatifu wa Israeli.

15. Nitawafanya muwe kama chombo cha kupuria,chenye meno mapya na makali.Mtaipura milima na kuipondaponda;vilima mtavisagasaga kama makapi.

16. Mtaipepeta milima hiyo,nao upepo utaipeperushia mbali,naam, dhoruba itaitawanya huko na huko.Nanyi mtafurahi kwa sababu yangu Mwenyezi-Mungu;mtaona fahari kwa sababu yanguMungu Mtakatifu wa Israeli.

Kusoma sura kamili Isaya 41