Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 5:19-31 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Halafu kuhani atamwapisha mwanamke huyo akisema: ‘Ikiwa hukulala na mwanamume mwingine, ukajitia najisi hali uko chini ya mamlaka ya mumeo, basi, hutapatwa na laana iletwayo na maji haya machungu.

20. Lakini kama umepotoka hali uko chini ya mamlaka ya mumeo, ukajitia najisi kwa kulala na mwanamume mwingine asiye mume wako,

21. Mwenyezi-Mungu na akuadhibu hata uwe laana na apizo miongoni mwa watu wako, uwe tasa na tumbo lako livimbe.

22. Maji haya yaletayo laana na yaingie tumboni mwako na kukufanya tasa na tumbo lako livimbe.’ Naye mwanamke ataitikia, ‘Amina, Amina.’

23. “Kisha kuhani ataandika laana hizi kitabuni na kuzioshea katika maji machungu;

24. naye atamnywesha mwanamke hayo maji machungu yaletayo laana nayo yataingia ndani yake na kumletea maumivu makali;

25. kisha kuhani atachukua ile sadaka ya nafaka ya wivu mikononi mwa mwanamke huyo na kuitikisa mbele ya Mwenyezi-Mungu, na kuipeleka madhabahuni.

26. Halafu, atatwaa konzi moja ya sadaka hiyo ya nafaka kwa ukumbusho na kuiteketeza madhabahuni. Hatimaye atamnywesha mwanamke maji hayo.

27. Akisha kunywa, kama amejitia najisi na hakuwa mwaminifu kwa mume wake, maji hayo yaletayo laana yatamletea maumivu makali sana; mwili wake utavimba na tumbo lake la uzazi litaharibika. Mwanamke huyo atakuwa laana miongoni mwa watu wake.

28. Lakini kama mwanamke huyo hajajitia unajisi na hana hatia, basi hatadhurika na ataweza kupata watoto.

29. “Basi, hii ndiyo sheria kuhusu kesi za wivu iwapo mwanamke, ingawa yu chini ya mamlaka ya mumewe, atapotoka na kujitia unajisi,

30. au wakati mwanamume ashikwapo na wivu na kumshuku mkewe. Atamsimamisha mwanamke huyo mbele ya Mwenyezi-Mungu, na kuhani atatekeleza masharti yote ya sheria hii.

31. Mumewe hatakuwa na hatia yoyote, lakini mwanamke atawajibika kwa uovu wake.”

Kusoma sura kamili Hesabu 5