Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 22:29-41 Biblia Habari Njema (BHN)

29. Balaamu akamwambia punda, “Wewe umenidhihaki! Kama ningekuwa na upanga ningalikuulia mbali sasa hivi!”

30. Punda akamwambia Balaamu, “Je, mimi si yuleyule punda wako aliyekubeba maisha yako yote hadi siku hii ya leo? Je, nimewahi kukutendea namna hii?” Balaamu akajibu, “La.”

31. Hapo, Mwenyezi-Mungu akayafungua macho ya Balaamu, naye akamwona malaika wa Mwenyezi-Mungu amesimama njiani, ameshika upanga uliochomolewa alani mwake. Balaamu akajitupa chini kifudifudi.

32. Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Balaamu, “Mbona umempiga punda wako mara hizi tatu? Nimekuja kukuzuia, kwa sababu njia yako ni mbaya.

33. Punda wako ameniona akaniepa mara hizi tatu. Kama asingaligeuka mbali nami hakika ningalikuua wewe na kumwacha hai punda huyu.”

34. Balaamu akamwambia malaika wa Mwenyezi-Mungu “Nimetenda dhambi maana sikujua kwamba umesimama njiani kunizuia. Sasa, kama haikupendezi niendelee na safari hii, basi nitarudi nyumbani.”

35. Lakini malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia Balaamu, “Nenda na watu hawa, lakini utasema tu kile nitakachokuambia.” Basi, Balaamu akaendelea na safari pamoja na viongozi wa Balaki.

36. Balaki alipopata habari kwamba Balaamu anakuja, alitoka kwenda kumlaki mjini Ari, mji uliokuwa ukingoni mwa mto Arnoni kwenye mpaka wa Moabu.

37. Balaki akamwambia Balaamu, “Kwa nini hukuja kwangu mara moja nilipokuita? Je, ulifikiri sitaweza kukutunukia heshima ya kutosha?”

38. Balaamu akamjibu Balaki, “Sasa nimekuja! Lakini, je, nina mamlaka ya kusema chochote tu? Jambo atakaloniambia Mungu ndilo ninalopaswa kusema.”

39. Basi, Balaamu akaenda pamoja na Balaki wakafika mjini Kiriath-husothi.

40. Huko Balaki alitoa kafara ya ng'ombe na kondoo, akawagawia nyama Balaamu na maofisa waliokuwa pamoja naye.

41. Kesho yake, Balaki alimchukua Balaamu, akapanda naye mpaka Bamoth-baali; kutoka huko, Balaamu aliweza kuwaona baadhi ya Waisraeli.

Kusoma sura kamili Hesabu 22