Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 21:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mfalme mmoja Mkanaani wa Aradi aliyeishi huko Negebu alipopata habari kwamba Waisraeli walikuwa wanakuja kwa njia ya Atharimu, alikwenda kuwashambulia, akawateka baadhi yao.

2. Hapo, Waisraeli wakamwekea Mwenyezi-Mungu nadhiri wakisema: “Kama utawatia watu hawa mikononi mwetu, basi tutaiangamiza kabisa miji yao.”

3. Mwenyezi-Mungu akalisikia ombi lao, akawapa ushindi juu ya Wakanaani. Waisraeli wakawaangamiza kabisa Wakanaani pamoja na miji yao. Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Horma.

4. Waisraeli walifunga safari kutoka Mlima Hori wakapitia njia inayoelekea bahari ya Shamu ili waizunguke nchi ya Edomu. Lakini njiani watu walikufa moyo.

5. Basi, wakaanza kumnungunikia Mungu na Mose, wakisema, “Kwa nini mmetutoa Misri tuje tukafie humu jangwani? Humu hamna chakula wala maji; nasi tumechoshwa na chakula hiki duni.”

6. Hapo Mwenyezi-Mungu akapeleka nyoka wenye sumu miongoni mwa watu, wakawauma hata Waisraeli wengi wakafa.

7. Basi, watu wakamwendea Mose, wakamwambia, “Tumetenda dhambi kwa kumnungunikia Mwenyezi-Mungu na wewe pia. Mwombe Mwenyezi-Mungu atuondolee nyoka hawa.” Kwa hiyo, Mose akawaombea watu.

8. Ndipo Naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Tengeneza nyoka wa shaba, umtundike juu ya mlingoti. Mtu yeyote atakayeumwa na nyoka, akimtazama nyoka huyo wa shaba, atapona.”

9. Basi, Mose akatengeneza nyoka wa shaba, akamtundika juu ya mlingoti. Kila mtu aliyeumwa na nyoka alipomtazama nyoka huyo wa shaba, alipona.

10. Waisraeli waliendelea na safari yao, wakapiga kambi huko Obothi.

11. Kutoka huko walisafiri mpaka Iye-abarimu, katika jangwa upande wa mashariki, mwa Moabu.

12. Kutoka huko walisafiri wakapiga kambi yao katika bonde la Zeredi.

Kusoma sura kamili Hesabu 21