Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 20:2-12 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Mahali hapo walipopiga kambi hapakuwa na maji. Kwa hiyo watu jumuiya yote, wakakusanyika kinyume cha Mose na Aroni.

3. Waliwalalamikia wote wakisema, “Afadhali tungekufa pamoja na ndugu zetu mbele ya hema la Mwenyezi-Mungu!

4. Kwa nini mlituleta sisi jumuiya ya Mwenyezi-Mungu huku jangwani? Je, mlituleta ili tufe pamoja na mifugo yetu?

5. Na, kwa nini mlitutoa Misri na kutuleta mahali hapa pabaya hivi? Hapa si mahali pa nafaka, tini, zabibu wala makomamanga. Hata maji ya kunywa hakuna!”

6. Hapo, Mose na Aroni waliondoka kwenye umati wa watu, wakaenda kusimama kwenye mlango wa hema la mkutano, wakasujudu. Basi, utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukawatokea,

7. naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,

8. “Twaa ile fimbo yako, kisha wewe na Aroni ndugu yako, muikusanye jumuiya yote ya watu. Halafu, mbele ya macho yao, uuambie mwamba ulio mbele ya macho yao utoe maji yake. Naam, utaufanya mwamba utoe maji, ili jumuiya nzima ya watu na mifugo yao waweze kunywa.”

9. Mose akaenda kuichukua ile fimbo mbele ya Mwenyezi-Mungu kama alivyoamriwa.

10. Kisha Mose na Aroni wakaikusanya jumuiya yote ya watu mbele ya mwamba, naye Mose akawaambia, “Sikilizeni sasa, enyi waasi: Je, tuwatoleeni maji kutoka mwamba huu?”

11. Kisha Mose akainua mkono wake, akaupiga ule mwamba mara mbili kwa fimbo yake. Maji yakabubujika kwa wingi, watu wakanywa pamoja na mifugo yao.

12. Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, “Kwa kuwa nyinyi hamkuniamini mimi, wala kunistahi mbele ya macho ya Waisraeli, basi kwa sababu hiyo hamtaiingiza jumuiya hii katika ile nchi niliyowapa.”

Kusoma sura kamili Hesabu 20