Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 13:25-33 Biblia Habari Njema (BHN)

25. Baada ya kuipeleleza nchi kwa muda wa siku arubaini, watu hao walirudi.

26. Waliwaendea Mose, Aroni na jumuiya ya Waisraeli huko Kadeshi, katika jangwa la Parani, wakatoa taarifa ya mambo waliyoyaona na kuwaonesha matunda ya nchi.

27. Walimwambia Mose, “Tuliifikia nchi uliyotutuma tuipeleleze; hiyo ni nchi inayotiririka maziwa na asali, na hili ni tunda lake.

28. Lakini wenyeji wake ni wenye nguvu sana, na miji yao ni imara na mikubwa sana. Zaidi ya hayo, huko tuliona wazawa wa Anaki.

29. Waamaleki wanakaa katika eneo la Negebu; Wahiti, Wayebusi na Waamori wanakaa katika eneo la milima, na Wakanaani wanakaa karibu na bahari ya Mediteranea na karibu na kingo za mto Yordani.”

30. Lakini Kalebu aliwanyamazisha watu mbele ya Mose, akasema, “Twende mara moja tukaimiliki nchi hiyo. Kwa kuwa tunao uwezo sana wa kushinda.”

31. Lakini watu walioandamana naye kuipeleleza nchi wakasema, “Hatutaweza kupigana na watu hao; wao wana nguvu kuliko sisi.”

32. Kwa hiyo wakaeneza mambo ya uongo kati ya wana wa Israeli kuhusu nchi waliyoipeleleza, wakisema, “Nchi hiyo inawaua watu wake. Pia watu wote tuliowaona huko ni wakubwa sana.

33. Tuliona majitu huko, wazawa wa Anaki. Sisi tulijiona kuwa kama panzi mbele yao, na ndivyo walivyotuona sisi.”

Kusoma sura kamili Hesabu 13