Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 11:21-31 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Lakini Mose alimwambia Mwenyezi-Mungu, “Idadi ya watu ninaowaongoza hapa ni 600,000 waendao kwa miguu, nawe wasema, ‘Nitawapa nyama ya kuwatosha mwezi mzima!’

22. Je, panaweza kuchinjwa kondoo na ng'ombe wa kuwatosheleza? Je, samaki wote baharini wavuliwe kwa ajili yao?”

23. Mwenyezi-Mungu akamjibu Mose, “Je, uwezo wangu umepungua? Utaona basi kama neno langu litakuwa la kweli kwako au la.”

24. Basi, Mose akaenda na kuwajulisha watu yale aliyosema Mwenyezi-Mungu. Kisha, akakusanya wazee sabini kutoka miongoni mwa wazee viongozi nao akawaweka kandokando kuizunguka hema.

25. Hapo, Mwenyezi-Mungu akashuka katika wingu na kuzungumza naye. Halafu akatwaa sehemu ya roho aliyokuwa amempa Mose, akawapa kila mmoja wa wale wazee sabini. Walipoingiwa na roho hiyo, wazee hao walianza kutoa unabii, lakini hawakurudia kufanya hivyo.

26. Wazee wawili kati ya wale sabini waliochaguliwa, Eldadi na Medadi, walikuwa wamebaki kambini wenzao walipokwenda kwenye hema. Roho iliwajia humohumo kambini, wakaanza kutoa unabii mahali walipokuwa.

27. Kijana mmoja alitoka mbio na kumwambia Mose, “Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini.”

28. Hapo, Yoshua, mwana wa Nuni, ambaye alikuwa msaidizi wa Mose tangu ujana wake, akamwambia Mose, “Bwana wangu, wakataze!”

29. Lakini Mose akamjibu, “Je, unaona wivu kwa ajili yangu? Laiti Mwenyezi-Mungu angewapa watu wake wote roho yake nao wakawa manabii!”

30. Kisha Mose alirudi kambini pamoja na wale wazee sabini wa Israeli.

31. Baadaye Mwenyezi-Mungu akavumisha upepo kwa ghafla, ukaleta kware kutoka baharini na kuwafanya watue kando ya kambi, mwendo wa siku moja hivi kila upande kuizunguka kambi, wakarundikana chini karibu kimo cha mita moja hivi.

Kusoma sura kamili Hesabu 11