Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 11:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Watu walianza kumlalamikia Mwenyezi-Mungu juu ya taabu zao. Mwenyezi-Mungu aliposikia, alishikwa na hasira, akawapelekea moto. Moto huo uliwaka kati yao na kuchoma upande mmoja wa kambi.

2. Watu wakamlilia Mose, naye akamwomba Mwenyezi-Mungu na moto huo ukazimika.

3. Kwa hiyo, mahali hapo pakaitwa Tabera, kwa sababu hapo moto wa Mwenyezi-Mungu uliwaka kati ya watu.

4. Miongoni mwa Waisraeli kulikuwa na kundi fulani lililoandamana nao ambalo lilikuwa na hamu kubwa. Waisraeli kwa mara nyingine walilia, wakisema. “Laiti kama tungeweza kupata nyama ya kula!

5. Tunakumbuka, samaki tuliokula kule Misri bila malipo, matango, matikiti, mboga, vitunguu na vitunguu saumu!

6. Lakini sasa nguvu zimetuishia na hakuna chakula kingine isipokuwa hii mana tu!”

7. Mana ilikuwa kama punje za mtama, rangi yake ilikuwa kama ya bedoza.

8. Watu walizungukazunguka na kuikusanya, kisha waliisaga kwa mawe ya kusagia au waliitwanga kwa vinu, halafu waliitokosa vyunguni na kutengeneza maandazi. Ladha yake ilikuwa kama ya maandazi yaliyokaangwa kwa mafuta.

9. (Umande ulipoanguka kambini wakati wa usiku, mana pia ilianguka pamoja na huo umande).

10. Mose alisikia watu wakilia katika familia zote, kila mtu penye lango la hema lake. Basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwaka sana; naye Mose alichukizwa.

11. Ndipo Mose alipomwambia, Mwenyezi-Mungu “Kwa nini unanitendea vibaya mimi mtumishi wako? Mbona hupendezwi nami, kwa nini umenitwika mzigo wa kuwatunza watu wote hawa?

12. Je, ni mimi niliyewazaa, hata ukaniambia niwabebe kifuani pangu kama mlezi abebavyo mtoto mchanga, na kuwapeleka mpaka nchi uliyoapa kuwapa babu zao?

13. Nitapata wapi nyama ya kuwalisha watu hawa wote? Maana wanalia mbele yangu wakisema: ‘Tupe nyama tule!’

Kusoma sura kamili Hesabu 11