Agano la Kale

Agano Jipya

Ezra 9:10-15 Biblia Habari Njema (BHN)

10. “Lakini sasa, ee Mungu wetu, tuseme nini baada ya hayo yote? Maana, tumeziasi amri zako

11. ulizotupa kwa njia ya watumishi wako manabii ukisema: ‘Nchi mnayoiendea na ambayo itakuwa mali yenu ni nchi iliyo najisi yenye uchafu wa wakazi toka nchi mbalimbali, kwa machukizo yao, wameijaza unajisi tele kila mahali.

12. Kwa hiyo, msiwaoze watu hao binti zenu, wala msiwaruhusu wavulana wenu kuwaoa binti zao. Pia, msishughulikie usalama au mafanikio yao, ili nyinyi wenyewe muweze kuwa na nguvu, na mfaidi mema ya nchi hiyo na kuwaachia watoto wenu kama urithi milele.’

13. Hata baada ya yote yaliyotupata kwa sababu ya maovu yetu na makosa yetu mengi, tunajua kwamba adhabu uliyotupa, ee Mungu wetu, ni ndogo ikilinganishwa na makosa yetu, na umewaacha baadhi yetu hai.

14. Je, tutavunja amri zako tena na kuoana na watu hawa watendao maovu haya? Je, hutatukasirikia na kutuangamiza kabisa, asibaki hata mmoja wetu hai wala yeyote wa kutoroka?

15. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, wewe ni mwenye haki na umetuacha tubaki kama tulivyo hivi leo. Tunaungama makosa yetu mbele yako, tukijua kuwa hakuna aliye na haki yoyote ya kuja mbele yako kwa ajili ya makosa haya.”

Kusoma sura kamili Ezra 9