Agano la Kale

Agano Jipya

Ezra 6:8-20 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Zaidi ya hayo, natoa amri kwamba nyinyi mtawasaidia katika kazi hiyo. Gharama zao zote zitalipwa bila kuchelewa kutoka katika hazina ya mfalme inayotokana na kodi kutoka katika mkoa wa magharibi wa mto Eufrate.

9. Kila siku, tena bila kukosa, mtawapa makuhani wa Yerusalemu kila kitu watakachohitaji; iwe ni fahali wachanga, kondoo dume au wanakondoo wa sadaka za kuteketezwa kwa Mungu wa mbinguni, au ngano, chumvi, divai au mafuta.

10. Haya yote yatatendeka ili waweze kumtolea Mungu wa mbinguni tambiko zinazompendeza na waombee maisha yangu mimi mfalme na watoto wangu.

11. Naamuru pia kwamba mtu yeyote ambaye hatatii amri hii, boriti ingolewe kutoka katika nyumba yake, na atumbuliwe kwayo. Tena, nyumba yake na ifanywe kuwa rundo la mavi.

12. Mungu aliyeuchagua mji wa Yerusalemu kuwa mahali pake pa kuabudiwa na amwangushe mfalme au taifa lolote litakalopinga amri hii au kutaka kuiharibu nyumba hii ya Mungu iliyoko mjini Yerusalemu. Mimi Dario nimetoa amri hii. Ni lazima ifuatwe.’”

13. Basi, Tatenai, mtawala wa mkoa wa magharibi ya mto Eufrate, Shethar-bozenai, na maofisa wenzao, wakafanya bidii kutekeleza maagizo ya mfalme.

14. Viongozi wa Wayahudi waliendelea vizuri sana na kazi ya ujenzi wa hekalu, wakitiwa moyo kwa mahubiri ya nabii Hagai na Zekaria, mwana wa Ido. Walimaliza ujenzi wa hekalu kama walivyoamriwa na Mungu wa Israeli, na kama walivyoagizwa na mfalme Koreshi, mfalme Dario na mfalme Artashasta, wa Persia.

15. Ujenzi wa nyumba hiyo ulimalizika mnamo siku ya tatu ya mwezi wa Adari, katika mwaka wa sita wa utawala wa mfalme Dario.

16. Basi, watu wa Israeli, makuhani, Walawi na watu wengine waliokuwa wamerudi kutoka uhamishoni waliiweka wakfu nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa shangwe kuu.

17. Wakati wa kuiweka wakfu nyumba ya Mungu, walitoa mafahali 100, kondoo madume 200, wanakondoo 800 na mbuzi madume 12 kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi, mbuzi mmoja kwa kila kabila la Israeli.

18. Pia, kwa ajili ya huduma ya Mungu katika Yerusalemu, waliwapanga makuhani katika makundi yao ya Walawi katika zamu zao kufuatana na maagizo yaliyoandikwa katika kitabu cha Mose.

19. Mnamo siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, watu waliokuwa wamerudi kutoka uhamishoni walisherehekea Pasaka.

20. Makuhani na Walawi walikuwa wamejitakasa, wote walikuwa safi kabisa. Walichinja mwanakondoo wa Pasaka kwa ajili ya watu wote waliorudi kutoka uhamishoni, ndugu zao makuhani na kwa ajili yao wenyewe.

Kusoma sura kamili Ezra 6