Agano la Kale

Agano Jipya

Ezra 10:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Wakati Ezra alipokuwa anaomba na kuungama huku analia na kujiangusha kifudifudi mbele ya nyumba ya Mungu, umati mkubwa wa watu wa Israeli, wanaume, wanawake na watoto, walikusanyika karibu naye wakilia kwa uchungu mwingi.

2. Ndipo Shekania, mwana wa Yehieli, wa ukoo wa Elamu, akamwambia Ezra, “Tumekosa uaminifu kwa Mungu kwa kuoa wanawake wa kigeni wa nchi hii, lakini hata hivyo bado kuna tumaini kwa ajili ya Israeli.

3. Kwa hiyo, na tufanye agano na Mungu wetu, tuachane na wanawake hawa pamoja na watoto wao, kwa kufuatana na ushauri wako na wa wengine wanaotii amri za Mungu. Yote yatendeke kwa kufuatana na sheria.

4. Amka uchukue hatua, sisi tutakuunga mkono. Kwa hiyo jipe moyo ufanye hivyo.”

5. Ezra alianza kwa kuwafanya makuhani, viongozi, Walawi na Waisraeli wengine wote waape kwamba watafanya kama ilivyosemwa, nao wakakubali kula kiapo.

6. Kisha, Ezra akaondoka mbele ya nyumba ya Mungu, akaenda nyumbani kwa Yehohanani, mwana wa Eliashibu. Huko, Ezra alilala usiku kucha bila kula wala kunywa maji, kwa huzuni aliyokuwa nayo juu ya ukosefu wa imani ya watu waliotoka uhamishoni.

7. Tangazo lilitolewa kila mahali nchini Yuda na mjini Yerusalemu kwa wote waliotoka uhamishoni kuwa wakusanyike Yerusalemu.

8. Ikiwa mtu yeyote atashindwa kufika katika muda wa siku tatu, kulingana na amri iliyotolewa na viongozi, mali yake yote itachukuliwa, naye binafsi atapigwa marufuku kujiunga na jumuiya ya watu waliorudi kutoka uhamishoni.

9. Katika siku hizo tatu, mnamo siku ya ishirini ya mwezi wa tisa, watu wote walioishi katika Yuda na Benyamini walifika Yerusalemu na kukusanyika katika uwanja wa nyumba ya Mungu. Watu wote walikuwa wakitetemeka kwa sababu ya jambo waliloitiwa na kwa ajili ya mvua nyingi iliyokuwa ikinyesha.

10. Kuhani Ezra alisimama kuzungumza na watu, akawaambia: “Hamkuwa waaminifu kwa kuoa wanawake wa kigeni, na hivyo mmeiongezea Israeli hatia.

Kusoma sura kamili Ezra 10