Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 47:10-23 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Wavuvi watasimama ufuoni mwa bahari, na eneo kutoka Engedi mpaka En-eglaimu litakuwa la kuanikia nyavu zao. Kutakuwa na aina nyingi za samaki kama zilivyo katika Bahari ya Mediteranea.

11. Lakini sehemu zake zenye majimaji na mabwawa kando ya bahari, hazitakuwa na maji mazuri. Bali hayo yatabaki kuwa maji ya chumvi.

12. Kisha ukingoni mwa mto huo kutaota kila namna ya miti itoayo chakula. Majani yake hayatanyauka wala miti hiyo haitaacha kuzaa matunda. Itazaa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu inapata maji yanayotiririka kutoka maskani ya Mungu. Matunda yake yatakuwa chakula na majani yake yatatumika kuponya magonjwa.”

13. Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Hii ndiyo mipaka ya nchi mtakayoyagawia makabila kumi na mawili ya Israeli. Lakini kabila la Yosefu lipewe maradufu.

14. Nyote mtagawana sawa. Niliapa kuwa nitawapa wazee wenu nchi hii, nayo itakuwa mali yenu.

15. Upande wa kaskazini mpaka utapita kutoka Bahari ya Mediteranea, kuelekea mji wa Hethloni, hadi mahali pa kuingia Hamathi na kuendelea hadi Zedadi.

16. Kutoka hapo utaendelea hadi Berotha na Sibraimu (ulio kati ya Damasko na Hamathi), hadi mji wa Haser-hatikoni ulio mpakani mwa Haurani.

17. Hivyo mpaka utakwenda kutoka bahari ya Mediteranea kuelekea mashariki hadi mji wa Hasar-enoni ukipakana na maeneo ya Damasko na Hamathi kwa upande wa kaskazini.

18. Upande wa mashariki, mpaka utakuwa mto wa Yordani unaoelekea kati ya Haurani na Damasko, Gileadi na nchi ya Israeli. Pia mpaka utapitia upande wa mashariki wa Bahari ya Chumvi hadi Tamari.

19. Upande wa kusini, toka Tamari mpaka utaendelea hadi chemchemi ya Meriba-kadeshi. Kutoka Meriba-kadeshi mpaka utaelekea kusini-magharibi hadi Bahari ya Mediteranea ukipitia mashariki ya nchi ya Misri.

20. Upande wa magharibi, mpaka ni Bahari ya Mediteranea na utapanda kaskazini hadi mahali pa kuingilia Hamathi.

21. “Basi, mtagawanya nchi hii kati yenu kulingana na makabila ya Israeli.

22. Mtaigawanya kuwa mali yenu. Wageni watakaokaa kati yenu na wamezaa watoto, pia wapewe sehemu ya nchi mnapoigawanya. Hao ni lazima watendewe kama raia halisi wa Israeli na wana haki ya kupiga kura ili kupata sehemu ya nchi pamoja na makabila ya Israeli.

23. Kila mgeni anayekaa nanyi atapewa sehemu yake pamoja na watu wa kabila ambamo anaishi. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Kusoma sura kamili Ezekieli 47