Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 44:4-15 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Yule mtu akanipeleka mbele ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, kwa njia ya lango la kaskazini. Nilipoangalia, nikaona utukufu wa Mwenyezi-Mungu umeijaza nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Hapo nikaanguka kifudifudi.

5. Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Wewe mtu! Tia maanani mambo yote unayoona na kusikia. Nitakueleza kanuni na masharti ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Zingatia moyoni mwako kwa makini, ni watu gani wanaoruhusiwa kuingia na kutoka katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ni watu gani wamekatazwa kuingia humo.

6. Utawaambia hao watu waasi wa Israeli, Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: Siwezi kuendelea kuyavumilia machukizo yenu yote.

7. Mmeitia unajisi maskani yangu kwa kuruhusu waingie humo watu wasiotahiriwa, watu wasionitii mimi, wakati mafuta na damu vinatambikwa kwa ajili yangu. Hivyo, nyinyi watu wangu mmelivunja agano langu kwa machukizo yenu yote.

8. Badala ya kutekeleza huduma ya vitu vyangu vitakatifu, mmeruhusu watu wa mataifa mengine kutekeleza huduma hiyo katika maskani yangu.

9. Sasa, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Hakuna mtu yeyote wa taifa geni, asiyetahiriwa au asiyenitii mimi, atakayeruhusiwa kuingia maskani yangu; hata wageni wanaoishi miongoni mwa Waisraeli, hawataruhusiwa.

10. “Walawi walioniacha wakati ule Waisraeli walipojitenga nami kwa kufuata miungu yao, watabeba adhabu yao.

11. Wataweza tu kuhudumu katika maskani yangu kama watumishi wakilinda malango ya nyumba yangu, na kutumikia katika nyumba. Wataweza kuchinja wanyama wanaotolewa na watu kwa ajili ya tambiko za kuteketeza na kuwatumikia watu.

12. Lakini kwa sababu waliongoza ibada za miungu kwa ajili ya watu wa Israeli, wakawafanya watu kutenda dhambi, basi, nimeunyosha mkono wangu kuwaadhibu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Nao watabeba adhabu yao.

13. Hawatanikaribia tena kunihudumia kama makuhani, wala hawatavigusa tena vitu vitakatifu wala vile vitakatifu kabisa. Bali wataaibika kwa sababu ya machukizo yao waliyotenda.

14. Hata hivyo, watashika zamu ya kulinda nyumba, wakifanya huduma yote na kazi zote zitakazotendeka humo.

15. “Lakini makuhani wa kabila la Lawi ambao ni wazawa wa Sadoki walioendeleza kazi yangu katika patakatifu pangu, wakati Waisraeli waliponiacha, hao ndio watakaoendelea kunitumikia na kuja mbele yangu kunitolea mafuta na damu.

Kusoma sura kamili Ezekieli 44