Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 44:12-26 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Lakini kwa sababu waliongoza ibada za miungu kwa ajili ya watu wa Israeli, wakawafanya watu kutenda dhambi, basi, nimeunyosha mkono wangu kuwaadhibu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Nao watabeba adhabu yao.

13. Hawatanikaribia tena kunihudumia kama makuhani, wala hawatavigusa tena vitu vitakatifu wala vile vitakatifu kabisa. Bali wataaibika kwa sababu ya machukizo yao waliyotenda.

14. Hata hivyo, watashika zamu ya kulinda nyumba, wakifanya huduma yote na kazi zote zitakazotendeka humo.

15. “Lakini makuhani wa kabila la Lawi ambao ni wazawa wa Sadoki walioendeleza kazi yangu katika patakatifu pangu, wakati Waisraeli waliponiacha, hao ndio watakaoendelea kunitumikia na kuja mbele yangu kunitolea mafuta na damu.

16. Hao tu ndio watakaoingia katika maskani yangu, nao watakaribia kwenye madhabahu kunitumikia.

17. Lakini wanapoingia katika ua wa ndani, watavaa mavazi ya kitani; hawatavaa mavazi ya sufu watakapohudumu katika malango ya ua wa ndani na kwenye nyumba.

18. Watavaa vilemba vya kitani vichwani mwao, na suruali za kitani viunoni mwao; lakini bila mkanda wowote.

19. Watakapotoka kwenda kwenye ua wa nje kwa watu, watavua mavazi waliyovaa wakati walipokuwa wanahudumu na kuyaweka katika vyumba vitakatifu. Ni lazima wavae mavazi mengine, ili watu wasije wakawa najisi kwa kugusa mavazi yao.

20. “Hawatanyoa vichwa vyao wala kuacha nywele zao ziwe ndefu. Lakini watapunguza tu mashungi ya nywele zao.

21. Kuhani yeyote asinywe divai anapoingia ua wa ndani.

22. Kuhani yeyote asioe mwanamke mjane wala mwanamke aliyepewa talaka. Lakini atamwoa bikira ambaye ni mzawa wa Waisraeli au mwanamke aliyefiwa na mumewe aliyekuwa kuhani.

23. Makuhani watafundisha taifa langu kupambanua vitu vilivyo vitakatifu na visivyo vitakatifu, na kuwajulisha tofauti baina ya vitu vilivyo najisi na visivyo najisi.

24. Kukiwako ugomvi wataamua kadiri ya sheria zangu. Katika sikukuu zote watafuata amri zangu na sheria zangu, na kuzitakasa sabato zangu.

25. Hawatakaribia maiti ili wasijitie unajisi. Lakini wataweza kujitia unajisi kwa kumkaribia baba au mama au mtoto wa kike au wa kiume au dada yao asiyeolewa, aliyekufa.

26. Mmoja wao akisha jitia unajisi, atakaa hali hiyo kwa muda wa siku saba. Kisha atakuwa safi.

Kusoma sura kamili Ezekieli 44