Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 40:16-26 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Kulikuwa na matundu madogomadogo kwenye miimo ya nje ya vyumba vyote na hata kwenye kuta zilizotenganisha vyumba. Kulikuwa na michoro ya mitende kwenye miimo ya ndani iliyoelekea ukumbi wa kupitia.

17. Kisha yule mtu akanipeleka mpaka ua wa nje ya hekalu. Huko kulikuwa na vyumba thelathini kuuzunguka ukuta wa nje na mbele ya vyumba hivyo kulikuwa na sakafu ya mawe.

18. Sakafu hiyo ilitandazwa kuzunguka malango kwa kufuatana na urefu wa malango hayo; hiyo ilikuwa sakafu ya chini.

19. Baadaye, yule mtu akapima umbali wa njia iliyokuwa ikitoka kwenye ua wa ndani wa sehemu ya chini ikielekea nje ya ua huo, akapata mita 50.

20. Kisha, yule mtu akapima urefu na upana wa lango la upande wa kaskazini wa ua wa nje.

21. Kulikuwa na vyumba vitatu vya walinzi kila upande wa lango, vipimo vya miimo yake na matao yake vilikuwa kama vile vya lango la kwanza. Urefu wote wa ile njia ulikuwa kwa jumla mita 25 na upana wake mita kumi na mbili u nusu.

22. Chumba cha kuingilia na madirisha na matao yake, pia ile mitende iliyochorwa ukutani, vyote vilifanana na vile vya lango la mashariki. Hapo palikuwa na ngazi saba za kupandia kwenye lango, na matao yake yalikuwa mbele yake.

23. Kutoka hapo penye njia ya kuingilia ya kaskazini na kuvuka huo ua moja kwa moja kulikuwa na njia nyingine ya kuingilia iliyoelekea kwenye ua wa ndani, kama ilivyokuwa upande wa mashariki. Yule mtu alipima urefu wa kutoka njia mpaka njia, akapata mita 50.

24. Yule mtu akanichukua upande wa kusini; huko nako kulikuwako lango; alipima miimo yake na ukumbi na vipimo vyake vilikuwa sawa na miimo na kumbi nyingine.

25. Kulikuwa na madirisha pande zote kama ilivyokuwa katika vyumba vingine. Urefu wake ulikuwa mita 25 na upana wake mita kumi na mbili u nusu.

26. Kulikuwa na ngazi saba za kupandia kwenye njia hiyo ya kuingilia na mwishoni mwake kulikuwa na ukumbi uliokuwa mkabala na ua. Kulikuwa na michoro ya mitende kwenye kuta za ndani zilizokuwa mkabala na hiyo njia ya kuingilia.

Kusoma sura kamili Ezekieli 40