Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 33:16-26 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Dhambi zake zote alizotenda hapo awali hazitakumbukwa; yeye ametenda yaliyo ya haki na mema; kwa hiyo hakika ataishi.

17. “Lakini wananchi wenzako wasema ati: ‘Anachofanya Mwenyezi-Mungu si sawa!’ Kumbe kwa kweli wao ndio hawafanyi kilicho sawa.

18. Mtu mwadilifu akiacha uadilifu wake, akaanza kutenda uovu, atakufa kwa sababu ya uovu wake.

19. Na mtu mwovu akiacha uovu wake, akaanza kutenda mambo ya haki na mema ataishi kwa sababu ya matendo yake mema.

20. Lakini, nyinyi mwasema ati: ‘Anachofanya Mwenyezi-Mungu si sawa!’ Enyi Waisraeli, mimi nitamhukumu kila mmoja wenu kadiri ya matendo yake.”

21. Siku ya tano ya mwezi wa kumi, mwaka wa kumi na mbili wa uhamisho wetu, mtu mmoja aliyetoroka kutoka Yerusalemu alinijia, akasema: “Mji wa Yerusalemu umetekwa!”

22. Wakati alipofika huyo mtu ilikuwa asubuhi kumbe jana yake jioni mimi nilisikia uzito wa nguvu yake Mwenyezi-Mungu. Basi, huyo mkimbizi alipowasili kwangu kesho yake asubuhi, nikaacha kuwa bubu, nikaanza kuongea tena.

23. Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:

24. “Wewe mtu! Wakazi waliobaki katika miji iliyoharibiwa nchini Israeli wanasema, ‘Abrahamu alikuwa peke yake, hata hivyo, alipata kuimiliki nchi hii. Lakini sisi ni wengi; ni dhahiri tumepewa nchi hii iwe yetu!’

25. Basi, waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nyinyi mnakula nyama yenye damu, mnaziabudu sanamu za miungu yenu na kuua! Je, mnadhani mtapewa nchi hii iwe yenu?

26. Mnategemea silaha zenu, mnafanya mambo ya kuchukiza na kila mwanamume miongoni mwenu anatembea na mke wa jirani yake! Je, mnadhani mtapewa nchi hii iwe yenu?

Kusoma sura kamili Ezekieli 33