Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 22:8-27 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Wewe umedharau vyombo vyangu vitakatifu na kuzikufuru sabato zangu.

9. Kwako wamo wanaowasingizia wengine ili wauawe. Wakazi wako hushiriki chakula kilichotolewa kwa miungu milimani. Watu wako wanatenda ufisadi.

10. Kwako wamo watu ambao hulala na wake za baba zao. Huwanajisi wanawake katika siku zao za hedhi.

11. Wengine hufanya machukizo kwa kulala na wake za majirani zao. Wengine hulala na wake za watoto wao, na wengine hulala na dada zao.

12. Huko kwako kuna watu ambao huua kwa malipo. Umepokea riba na kuwalangua wenzako ili kujitajirisha, na kunisahau mimi kabisa! Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.

13. “Nimekunja ngumi yangu dhidi yako kwa sababu ya hiyo faida uliyopata kwa njia isiyo halali na kwa mauaji yaliyofanyika kwako.

14. Je, utaweza kustahimili kuwa hodari siku nitakapopambana nawe? Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema na nitayatekeleza hayo.

15. Nitakutawanya kati ya mataifa na kukutupatupa katika nchi nyingine. Nitaukomesha uchafu ulioko kwako.

16. Utajiweka najisi mbele ya mataifa mengine, lakini utatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”

17. Tena neno la Mwenyezi-Mungu likanijia:

18. “Wewe mtu! Waisraeli wamekuwa kwangu kama takataka. Wao ni kama takataka inayosalia wakati madini ya shaba, bati, chuma au risasi yanaposafishwa.

19. Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa kuwa nyinyi nyote mmekuwa takataka ya madini, mimi nitawakusanya pamoja mjini Yerusalemu.

20. Kama watu wanavyokusanya fedha, shaba, chuma, risasi na bati katika tanuri ili kuzisafisha kwa kuchoma moto, ndivyo ghadhabu na hasira yangu itakavyowakusanya huko na kuwayeyusha.

21. Nitawakusanya na kuwawasha moto kwa ghadhabu yangu; nanyi mtayeyushwa mkiwa humo mjini.

22. Kama fedha iyeyushwavyo katika tanuri, ndivyo mtakavyoyeyushwa humo mjini. Nanyi mtatambua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nimeimwaga ghadhabu yangu juu yenu.”

23. Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:

24. “Wewe mtu! Waambie Waisraeli kwamba nchi yao ni kama nchi ambayo haijanyeshewa mvua, imenyauka kwa sababu ya ghadhabu yangu ikawa kama ardhi bila maji.

25. Wakuu wenu ni kama simba anayenguruma araruapo mawindo yake. Wanaua watu, wanawanyanganya watu mali na johari, na kuongeza idadi ya wajane.

26. Makuhani wao wanavunja sheria zangu, na kukufuru vyombo vyangu vitakatifu. Hawapambanui kati ya vitu vitakatifu na vitu visivyo vitakatifu, wala hawawafundishi watu tofauti kati ya mambo yaliyo najisi na yaliyo safi. Wameacha kuzishika sabato zangu, na kunifanya nidharauliwe kati yao.

27. Viongozi wake waliomo mjini ni kama mbwamwitu wararuao mawindo yao; wanaua ili kujitajirisha visivyo halali.

Kusoma sura kamili Ezekieli 22