Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 22:24-31 Biblia Habari Njema (BHN)

24. “Wewe mtu! Waambie Waisraeli kwamba nchi yao ni kama nchi ambayo haijanyeshewa mvua, imenyauka kwa sababu ya ghadhabu yangu ikawa kama ardhi bila maji.

25. Wakuu wenu ni kama simba anayenguruma araruapo mawindo yake. Wanaua watu, wanawanyanganya watu mali na johari, na kuongeza idadi ya wajane.

26. Makuhani wao wanavunja sheria zangu, na kukufuru vyombo vyangu vitakatifu. Hawapambanui kati ya vitu vitakatifu na vitu visivyo vitakatifu, wala hawawafundishi watu tofauti kati ya mambo yaliyo najisi na yaliyo safi. Wameacha kuzishika sabato zangu, na kunifanya nidharauliwe kati yao.

27. Viongozi wake waliomo mjini ni kama mbwamwitu wararuao mawindo yao; wanaua ili kujitajirisha visivyo halali.

28. Manabii wake wanaficha maovu hayo kama mtu anapotia chokaa kwenye ukuta mbovu. Wanaona maono ya uongo na kutabiri udanganyifu mtupu, wakisema, ‘Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi,’ wakati mimi mwenyewe sijawaambia chochote.

29. Kila mahali nchini ni dhuluma na unyanganyi. Wanawadhulumu maskini na wanyonge, na kuwaonea wageni bila kujali.

30. Nilitafuta miongoni mwao mtu mmoja atengeneze ukuta na kusimama juu ya mahali palipobomoka mbele yangu, ili ailinde nchi na kunizuia nisiiharibu, lakini sikumpata hata mmoja.

31. Kwa hiyo nimewamwagia ghadhabu yangu na kwa moto wa hasira yangu nimewateketeza kulingana na matendo yao. Ndivyo nisemavyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu.”

Kusoma sura kamili Ezekieli 22